KIKOSI MAALUM CHA MAKOMANDOO WA JWTZ KUPAMBA SHEREHE ZA MIAKA 53 YA MUUNGANO

Na: Lilian Lundo - MAELEZO.
Maonesho ya ukakamavu na mbinu za medani katika kupambana na adui hasa kulinda amani ya nchi yetu kutoka Kikosi Maalum cha Makomandoo wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), itakuwa ni sehemu ya shamrashamra zitakazopamba maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano yatakayofanyika kwa mara ya kwanza mjini Dodoma Aprili 26 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli, pia yatapambwa na burudani nyingine kutoka vikundi mbalimbali.

Taarifa ya Waziri Mhagama ametaja shughuli nyingine zinazotarajiwa kufanyika siku ya Muungano kuwa ni gwaride la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama (JWTZ,JKT, Polisi na Magereza) na onesho la mbwa na farasi waliofunzwa.

Aidha, Waziri Mhagama aliongeza kuwa mambo mengine yatakayofanyika ni gwaride la uzalendo la wanafunzi wa shule za sekondari za Dodoma, burudani za vikundi vya ngoma za asili kutoka Dodoma na Zanzibar, Yamoto Band, vikundi vya muziki wa kizazi kipya kutoka kwa wasanii Mchungaji Zayumba, Jacob Beats, Mwenge Jazz Band na Mgosi Maturumbeta.

“Kauli mbiu ya sherehe za kutimiza miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni Miaka 53 ya Muungano; Tuulinde na Kuumarisha, Tupige Vita Dawa za Kulevya na Kufanya Kazi kwa Bidii,”alifafanua Waziri Jenista Mhagama.

Ametoa wito kwa wananchi wote nchini kusherehekea siku hiyo muhimu kwa kudumisha amani, upendo, umoja na mshikamano kwa maendeleo ya nchi.

“Ninaomba kuchukua nafasi ya pekee kuwaomba wananchi wote waliopo Dodoma kujitokeza kwa wingi uwanja wa Jamhuri siku hiyo ya Jumatano tarehe 26 Aprili 2017 kuanzia saa 12:00 asubuhi ili kusherehekea kwa pamoja maadhimisho hayo muhimu kwa nchi yetu,”alisema Jenista Mhagama.

Maadhimisho ya Muungano yanafanyika kwa mara ya kwanza Dodoma ikiwa ni siku kadhaa tangu Serikali ya Awamu ya Tano ianze kutumiza azma ya kuhamia katika makao makuu hayo mapya

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post