Kushoto ni Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Muliro Jumanne Muliro akiwa ameshikilia bango la uzinduzi wa huduma ya wananchi kupiga simu bure kwa jeshi la polisi kufichua vitendo vya uhalifu katika jamii.Wa kwanza kulia ni Mkuu Wa idara ya utawala Halotel mkoa wa Shinyanga Throng Khoa na mkuu wa idara ya Ufundi Halotel mkoa wa Shinyanga Bw.Thao.
******
Kampuni ya mtandao wa simu za mkononi ya Halotel Tanzania imetambulisha huduma ya wananchi kupiga simu bure na kutoa taarifa za kuzuia na kupambana na uhalifu kwa jeshi la polisi hali itakayosaidia ustawi wa jamii mkoani Shinyanga.
Akizungumza baada ya makabidhiano ya simu moja ya mkononi na utambulisho wa namba 111 ambayo ni maalum itakayotumiwa na wananchi kutoa taarifa za uhalifu,Makamu Mkurugenzi wa Halotel mkoa wa Shinyanga,Alex Mushi amesema pamoja na kufichua vitendo vinavyohatarisha amani, lengo kubwa la kampuni hiyo ni kuwaondolea watanzania mzigo wa kupiga simu kwa malipo.
Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga SACP Muliro Jumanne Muliro amesema vitendo vya uhalifu mkoani hapa vimeendelea kupungua siku hadi siku kutokana na ushirikiano ambao jeshi hilo limekuwa likiupata kutoka kwa vyombo vingine vya ulinzi na usalama lakini zaidi ni wananchi wenyewe kuvichukia.