JWTZ WAJISALIMISHA TANESCO BAADA YA KUPEWA NOTISI YA KUKATIWA UMEME VITUO VYOTE

Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekiri kudaiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Sh bilioni tatu na kwamba linatarajia kuanza kupunguza kiasi cha deni hilo kwa kwa kuanza kulipa Sh bilioni moja leo.


Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Majeshi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo ambaye alibainisha wazi kuwa tayari Tanesco wamelipatia jeshi notisi ya kukatiwa umeme katika vituo vyake vyote leo, endapo deni hilo lisipolipwa.

“Hivi karibuni tumepokea taarifa ya Tanesco kuhusu kusitisha huduma kwenye vituo vyetu vyote kesho (leo) kutokana na deni kubwa tunalodaiwa. Hii ni kutokana na agizo la Rais John Magufuli kwa shirika hilo, kuwa liwakatie huduma wale wote wanadaiwa na shirika hilo,” alifafanua Jenerali Mabeyo.

Alikiri kuwa jeshi hilo linadaiwa na Tanesco zaidi ya Sh bilioni tatu na kufafanua kuwa kiwango hicho kikubwa cha deni kinatokana na matumizi makubwa ya umeme kwa sababu ya mtawanyiko wa jeshi hilo sehemu mbalimbali nchini, lakini pia matumizi ya umeme katika mitambo na zana ambazo nyingine hutumia umeme saa 24 kwa ajili ya usalama wa nchi.

Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo ya Tanesco, jeshi hilo lilitafakari na kuamua kupunguza deni lake.

“Tayari nimeagiza watendaji wetu watafute kiasi cha Sh bilioni moja ili kesho (leo) hundi ipelekwe haraka Tanesco kwa ajili ya malipo, na kuzuia tusikatiwe umeme,” alieleza.

Alibainisha kuwa pamoja na deni hilo la Tanesco, pia JWTZ inadaiwa na wazabuni wengine na tayari Hazina imeanza kulipatia jeshi hilo fedha kidogo kidogo ili kupunguza madeni hayo (hakutaja kiasi).

“Napenda nichukue fursa hii kuwakumbusha kuwa suala la ulinzi wa taifa halina mbadala, kusitisha huduma yoyote kwa JWTZ kunahatarisha usalama wa taifa. Tunaomba wanaotuhudumia wazingatie hili na kutuvumilia pale tunapolipa kidogo kutokana na changamoto ya ufinyu wa bajeti,” alisema Jenerali Mabeyo ambaye aliteuliwa na Rais Magufuli kushika wadhifa huo Februari 2, mwaka huu.

Aidha, alieleza kuwa pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali za kifedha, jeshi hilo limejipanga kuboresha vyanzo vyake vya mapato kama vile Suma JKT, Mzinga na Nyumbu kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali hali itakaloliwezesha jeshi hilo kujitegemea.

Alieleza kuwa jeshi hilo linaandaa waraka kwa ajili ya kuuwasilisha kwa Baraza la Mawaziri unaohusu namna ya kuiboresha Nyumbu. “Tuna imani hili litazingatiwa, kwani tukiweza kujitegemea tutaondokana na mzigo wa madeni unaotukabili,” alifafanua.

Jenerali Mabeyo alitumia fursa hiyo kuwahamasisha pia wadaiwa wengine sugu wa Tanesco, kuiga mfano wa jeshi hilo na kuanza kulipa madeni yao ili kuliwezesha shirika hilo kujiendesha na kutoa huduma bora ya umeme kwa watanzania.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo hivi karibuni wakati akizindua ujenzi wa mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme wa kilovolti 132 mkoani Mtwara ambacho kitaboresha upatikanaji wa umeme kwenye mikoa ya Mtwara na Lindi.

Baada ya agizo hilo la Rais Magufuli, Tanesco ilitoa muda wa siku 14, kuanzia Machi 9, mwaka huu kwa wateja wake wote linalowadai kulipa madeni yao, vinginevyo litasitisha utoaji wa huduma ya nishati kwa wahusika.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Dk Tito Mwinuka alisema shirika linadai jumla ya Sh bilioni 275.38. Kati ya fedha hizo, Wizara na Taasisi za Serikali zinadaiwa zaidi ya Sh bilioni 52.53, Shirika la Umeme Zanzibar, (ZECO), linadaiwa zaidi ya Sh bilioni 127.87, na kampuni binafsi na wateja wadogo wadogo deni ni zaidi ya Sh bilioni 94.97.

Tayari ZECO nao wameshapunguza kiasi cha Sh bilioni 10 kati ya Sh bilioni 127.67 ambalo shirika hilo linadaiwa na Tanesco.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post