BUNGE LAJITOSA SAKATA LA MCHANGA WA DHAHABU HUKU KATIBU WA WIZARA YA NISHATI NA MADINI AKITUMBULIWA

SPIKA wa Bunge, Job Ndugai ametangaza kuunda kamati teule itakayochunguza biashara ya kusafirisha nje ya nchi ‘mchanga wa dhahabu’ unaofanywa na wawekezaji wa mgodi wa Bulyanhulu na Buzwagi.

Akizungumza baada ya kutembelea makontena zaidi ya 260 yaliyozuiwa Bandari ya Dar es Salaam, Ndugai alisema Bunge litaunda kamati hiyo na ataitangaza hivi karibuni katika Mkutano wa Bajeti uliopangwa kuanza Aprili 4, mwaka huu.
“Nitatangaza muundo, mamlaka yake na hadidu za rejea... itafanya na mambo mengine ambayo kamati itahitaji kuyajua,” alieleza Ndugai.
Alisema wamelazimika kuunda kamati hiyo kutokana na utata uliopo katika biashara hiyo ya makinikia ya shaba maarufu kama mchanga wa dhahabu.
Alisema Watanzania wanahitaji kujua biashara hiyo ya mchanga wa dhahabu inafanywa vipi, nani wanafaidika na biashara hiyo ambayo usafirishaji wake nje ya nchi ulianza tangu mwaka 1998.
Alisema licha ya kuchunguza biashara hiyo, kamati pia itafanya uchunguzi juu ya uwekezaji wote wa madini na namna Watanzania wanavyofaidika.
Alisema kuita mchanga wa dhahabu ni kupotosha, kwani mchanga huo una madini ya dhahabu, shaba na fedha.
Alisema kwa mujibu wa wataalamu, dhahabu ni kidogo kwenye mchanga huo, lakini akasema kama ni kidogo kwa nini wawekezaji wanapeleka maelfu ya makontena nje ya nchi.
“Tunachojiuliza kama kweli dhahabu ni asilimia 0.02, mwekezaji anayeangalia dhahabu kwa nini akazanie kusafirisha makontena haya nje ya nchi kwa miaka 20 sasa? Alihoji Ndugai na kueleza kuwa, lazima kuna wizi fulani unafanyika.
Alisema umefika wakati wa kuchukua hatua kulinda rasilimali za nchi na akatolea mfano kuwa wawekezaji wa dhahabu wanalipa kodi kidogo, ambayo nayo baadaye wanarudishiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA), jambo ambalo linafanya nchi kubaki na kodi kidogo kutoka kwa wawekezaji hao.
Spika Ndugai alisema kwa mujibu wa takwimu za Wakala wa Madini Tanzania (TMAA), kila mwaka kontena zaidi ya 50,000 zinasafirishwa nje ya nchi, jambo ambalo linafanya tangu mwaka 1998 makontena zaidi ya milioni moja kuwa yameshasafirishwa nje ya nchi.
“Tungependa kujua ni nani anasimamia biashara hiyo kuanzia kwenye source (chanzo), hadi huko mchanga unakokwenda, nani anasimamia maslahi yetu huko China, Ujerumani au Japan ambako mchanga unapelekwa... utapelekaje mali yako wakati hakuna mtu anayekuangalizia? alihoji Ndugai.
Alisema muda umefika wa kuchukua hatua hasa wanapoona utajiri wa nchi unaondoka kwenda nje ya nchi.
Alisema Watanzania wanaendelea kuwa masikini na kuwa na bajeti tegemezi, wakati madini haya yangepata thamani halisi, nchi isingehitaji msaada kutoka nje ya nchi.
Alisema serikali ifanye wajibu wake wa kufuatilia kuhusu biashara hiyo, lakini Bunge lenyewe litachukua nafasi ya kuunda kamati itakayokuja na ushauri mzuri zaidi kuhusu suala hilo.
TPA yaishangaa
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Deusdedit Kakonko alisema wamelazimika kuzuia makontena hayo kusafirishwa nje ya nchi kutokana na agizo la Rais John Magufuli na kuzuia usafirishaji huo.
Alisema anayofahamu yeye agizo la Rais ni kama sheria, lakini akashangaa inakuwaje licha ya agizo la mkuu wa nchi, mchanga huo wa madini bado unaendelea kupelekwa bandarini hapo ili usafirishwe.
“Kuna uwezekano tuna wafanyakazi wa mamlaka hizi zingine sio waadilifu, ndio maana hata hili agizo la Rais wanashindwa kulifanyia kazi,” alisema bosi huyo mkuu wa TPA na kueleza namna walivyonasa makontena hayo zaidi ya 250.
Alisema baada ya ziara ya Rais bandarini hapo, walinasa makontena hayo na baadhi yakiwa tayari kupakiwa kwenye meli.
Alisema anaamini kuwa ndani ya makontena hayo asilimia 90 ya mchanga ni dhahabu na sio shaba kama inavyodaiwa.
TMAA yakanusha
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Madini (TMAA), Gilay Shamika alisema kilichoko ndani ya makontena hayo asilimia 90 ni shaba, asilimia 0.02 ni dhahabu na fedha ni 0.08.
Akielezea mchakato wa kupakia mchanga huo, Shamika alisema wanachukua sampuli wao, mgodi na kule mchanga unakopelekwa, wakishajiridhisha kiasi cha madini kilichomo, wawekezaji wanalipa kodi TRA.
“Tukishajiridhisha tunalifunga kontena na kuweka alama yetu na ya TRA kama inavyoonekana kwenye kontena,” alisema Shamika.
Aliongeza kuwa wakala una uhakika kuwa mchanga huo unatawaliwa na shaba na sio dhahabu kama inavyodaiwa na mkurugenzi wa mamlaka ya usimamizi wa bandari.
Wizara yajitetea
Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa alitetea mchanga huo kusafirishwa nje na kueleza kuwa hapa nchini hakuna kiwanda cha mchanga.
Alisisitiza kuwa lengo la wizara ni kuwa na kiwanda cha kuchenjua mchanga huo nchini, lakini uwekezaji wake ni gharama na hawajampata mwekezaji.
Aliongeza kuwa wizara yake itafanya uchunguzi tena wa kutambua ukweli wa kilichomo ndani ya makontena hayo kutokana na kuwepo ubishi kati ya TPA na TMAA.
Alisema wataunda timu ya wataalamu ambayo itachukua sampuli upya kwa kontena zote zilizoko hapo bandarini na kwenda kuchunguza upya ili kujua zaidi kilichomo ndani ya mchanga huo.
Alisema timu hiyo ya wataalamu itahusisha pia vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kujiridhisha na majibu yatakayotolewa na maabara.
“Tunachukua ushauri wenu ndugu wabunge, tutaunda kamati kuchunguza tena upya kuhusu kiasi cha madini kilichomo kwenye mchanga huu,” alisema Profesa Ntalikwa wakati alipokuwa anajibu hoja mbalimbali za wabunge walioambatana na Spika Ndugai.
Hivi karibuni Rais Magufuli alifanya ziara bandari ya Dar es Salaam na kuoneshwa kuwepo kwa makontena ya mchanga. Rais alisisitiza kuwa hakuna kusafirisha mchanga huo nje ya nchi na wawekezaji waje wajenge kiwanda hicho nchini.
Katibu Mkuu Nishati na Madini atumbuliwa
Saa chache baada ya kutoka katika ziara hiyo ya Spika, taarifa ya Ikulu, ilieleza kuwa Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Katibu Mkuu, Profesa Ntalikwa kuanzia jana.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, nafasi ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo itajazwa baadaye.
Hivi karibuni, Rais Magufuli pia alitengua uteuzi na kumsimamisha kazi Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, Uledi Mussa.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi, kutenguliwa kwa uteuzi na kusimamishwa kazi kwa Uledi, kumechukuliwa ili kupisha uchunguzi zaidi dhidi yake kwa kutozingatiwa taratibu zinazotakiwa katika kushughulikia masuala ya uwekezaji.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post