MKUU WA SHULE YA SEKONDARI AJINYONGA...CHANZO UPWEKE BAADA YA ULEVI


MKUU wa Shule ya Sekondari Tumuli katika Wilaya ya Mkalama, mkoani Singida, Richard Makala (58) amejinyonga kwa kamba kutokana na kile kinachodhaniwa kuelemewa na upweke.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Debora Magiligimba, amesema mjini Singida kuwa, Makala alijinyonga jana saa 1 asubuhi.

Ameeleza kuwa Makala alikutwa amejinyonga kwa kutumia kamba iliyotengenezwa kwa vipande vya chandarua iliyofungwa juu ya mti umbali wa mita 130 kutoka nyumbani kwake.

Amesema, chanzo cha tukio hilo hakijajulikana na kwamba hakuna mtu au watu wanaoshikiliwa kutokana na tukio hilo na kuongeza kuwa polisi inaendelea na upelelezi kubaini kilichomsibu mwalimu huyo.

Hata hivyo, Mjumbe wa Bodi ya shule hiyo, Mabruki Ng’ui amelisema mwalimu huyo alikuwa anaishi peke yake kwa muda mrefu baada ya mkewe ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Tanzania (KKKT) Kitusha wilayani Iramba kuamua kutengana naye kutokana na unywaji pombe.

"Huyu bwana amekuwa kwenye ndoa ya jina tu maana mke wake amekuwa akiishi mbali naye kwa kipindi kirefu sana, amekuwa mpweke kwa muda mrefu mno huenda hicho ndicho kilichosababisha ajitoe roho yake," amesema Mjumbe huyo wa Bodi.

Makala ni mzaliwa wa kijiji cha Ndago, wilayani Iramba na anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwake.

Ameacha mjane na watoto watano.

IMEANDIKWA NA ABBY NKUNGU-HABARILEO SINGIDA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527