MKE WA BILIONEA MSUYA AACHIWA HURU SHTAKA LA MAUAJI

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo imewaachia huru mke wa marehemu bilionea Erasto Msuya, Mariam Mrita (41) na mwenzake waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji ya dada wa bilionea huyo, Anitha, baada ya upande wa mashitaka kushindwa kurekebisha hati ya mashitaka.

Hata hivyo, baada ya kuachiwa, Mrita na mshitakiwa mwenzake, mfanyabiashara Revocatus Muyela (40) walikamatwa na kupandishwa kwenye gari la Polisi lenye namba DD 73JZ-GP.

Awali, Wakili wa Serikali, Hellen Moshi alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa kuwa shauri lilikuja kwa ajili ya uamuzi na kwamba jalada liliitishwa Mahakama Kuu na kupewa siku tatu kwa ajili ya kubadilisha hati ya mashitaka.

Moshi alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), ameona hati hiyo iko sahihi kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).

Jumatatu wiki hii, mahakama ilitoa siku tatu kwa upande wa mashitaka kuhakikisha wanarekebisha hati ya mashitaka na kupangwa jana kwa ajili ya uamuzi.

Wakili wa utetezi, Peter Kibatala alidai wanachokifanya upande wa mashitaka ni ukaidi kwa kuwa wamepewa muda wa kutosha na amri ya mahakama ipo wazi kwamba wasipofanya marekebisho itachukua hatua.

Alidai kwa kuwa hakuna rufaa yoyote, DPP amepinga uamuzi huo hivyo waachiwe huru. Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mwambapa alisema Januari 7, mwaka huu, mahakama iliamua upande wa mashitaka ufanye marekebisho mara baada ya kuona hati hiyo ina mapungufu lakini hawakufanya hivyo.

Alisema waliongezewa muda kwa ajili ya kufanya marekebisho hayo, hata hivyo wanakuja na kudai kuwa hati ni sahihi.

“Ni hati ipi ambayo iko sahihi wakati mahakama ilishasema haipo sahihi. Nawaachia huru washitakiwa wote,” alisema Hakimu Mwambapa.

Katika mashauri yaliyopita, upande wa utetezi uliomba mahakama kuwaachia huru washitakiwa hao kwa kuwa hati ya mashitaka haioneshi walivyoshiriki kufanya makosa hayo.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa wote wanadaiwa kumuua kwa makusudi dada wa bilionea huyo, Anitha kwa kumchinja nyumbani kwake eneo la Kibada Kigamboni, Mei 25, mwaka jana. Bilionea Msuya aliuawa kwa risasi Agosti, 2015 eneo la Mijohoroni kando ya Barabara ya Arusha – Moshi Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527