WACHIMBAJI : MUUJIZA UMETUOKOA KUFA MGODINI..SIMULIZI YAO INASIKITISHA



WACHIMBAJI madini 15 waliofukiwa mgodini katika kata ya Nyarugusu wilaya ya Geita mkoa wa Geita na kupelekwa hospitali ya mkoa huo juzi, waliruhusiwa jana.

Waliruhusiwa baada ya kupata matibabu huku baadhi ya ndugu zao wakionekana kushangazwa na hatua hiyo.

Katika muda wa chini ya saa 24 waliyokuwa wanapata matibabu hospitalini, manusura hao vijana walionekana kuwa na furaha tele.

Waliishukuru serikali na wadau wengine, kwa kuchukua hatua za haraka, zilizofanikisha kuokoa maisha yao.

Alipokutana nao muda mfupi baada ya kutolewa wodini, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali mstaafu, Ezekiel Kyungu alipongeza viongozi wa hospitali ya mkoa kwa kuwatibu manusura wa ajali hiyo baada ya kutolewa kutoka mgodini chini ya umbali wa mita 60 huku wakiwa wanakabiliwa na njaa.

‘’Tunamshukuru Mungu kwamba mko salama baada ya ajali mliyopata ambayo ilishtuakila mmoja wetu. Nimearifiwa kwamba mmepatiwa matibabu yenye weledi wa kutosha, kiasi kwamba sasa mnarejea nyumbani mkiwa na afya njema, nachukua nafasi hii kumshukuru kila mmoja aliyeshiriki katika operesheni ya uokozi,’’ alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, serikali imeshatoa maelekezo kwa mgodi husika, unaomilikiwa kwa ushirikiano kati ya mwekezaji kutoka China, RZ Union Mining Ltd na Mtanzania, Ahmed Mubarak kuendelea kufungwa kwa muda wa siku tano, ukisubiri uchunguzi unaoendelea juu ya nini kilichosababisha ajali hiyo na mbinu za kufanya ili kuzuia ajali kama hiyo.

Alisema tukio la ajali ya Nyarugusu, pia limeiamsha serikali kuchukua hatua za kukabiliana na hali ya operesheni dhidi ya wachimbaji wadogo na wa kati mkoani Geita haraka iwezekanavyo kuhusu hatua za usalama.

Alikuwa ananukuu maelekezo yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani aliyetembelea mkoa huo Jumapili baada ya ajali katika mgodi huo wa Nyarugusu.

Hatua nyingine kali ya serikali itafuatia kwa wawekezaji wa madini, ambao sasa watatakiwa kutoa mikataba ya uhakika kwa wafanyakazi wao, ikiwa ni pamoja na kuweka kipengele cha kulipwa fidia, iwapo watapata ajali katika operesheni za uchimbaji wa madini.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mmoja wa maanusura wa ajali hiyo, Anicet Masanja alisema wamefanikiwa kuishi na kunusurika kwa siku nne kutokana na mwamba na hewa ndani ya shimo walilokuwemo ardhini, uliozuia mchanga kuwaporomokea walipokuwa wanapambana kutafuta njia ya kujiokoa.

‘’Isingekuwepo umbile zuri la mwamba na miundombinu kuwa imara, tungekuwa tunazungumza lugha nyingine leo. Kwa ujumla tunamshukuru Mungu kwa muujiza uliojitokeza na juhudi za hospitali ya mkoa na wadau wengine, zilizofanikisha kuokolewa maisha yetu,’’ alieleza Masanja.

Wakati huo huo, Wizara ya Nishati na Madini imesema inapenda kuufahamisha umma kuwa kazi ya kuwaokoa wachimbaji 15 waliofukiwa na kifusi Januari 26, mwaka huu kwenye mgodi wa dhahabu eneo la kijiji cha Mawemeru, Nyarugusu wilayani Geita limekamilika kwa mafanikio.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Nishati na Madini jana, ilieleza kuwa ajali ya kufukiwa wachimbaji hao iliyohusisha Watanzania 14 na raia mmoja wa China, ilitokea kwenye leseni ya uchimbaji wa kati wa madini ya dhahabu yenye Namba ML 492/2013, inayomilikiwa na Ahmed Mubarak Adam.

Chanzo cha ajali hiyo, kwa mujibu wa wizara hiyo, ilikuwa ni kuanguka kwa shafti ya mgodi huo na kufukiwa na kifusi wakati wachimbaji hao wakifanya kazi mgodini chini ya ardhi.

Akizungumza baada ya kuokolewa wachimbaji hao, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard amewashukuru wadau wote walioshiriki kwa hali na mali, kufukua kifusi na hatimaye kufanikiwa kuwatoa wachimbaji chini ya ardhi wakiwa hai.

Dk Kalemani aliwaomba Watanzania kuendelea na moyo huo, pale majanga kama haya yanapotokea. Pia, aliagiza ukaguzi wa kina, ufanyike kwenye migodi mingine ya wachimbaji wadogo na ya kati eneo la Nyarugusu na kwingineko nchini ili kuhakikisha kuwa migodi inakuwa salama kwa wachimbaji wa migodi husika.

IMEANDIKWA NA PIUS RUGONZIBWA,-habarileo GEITA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527