MTUMISHI WA UMMA ATAKAYESHINDWA KUWASILISHA CHETI AU INDEX NUMBER ATAKUWA AMEJIONDOA KAZINI MWENYEWE


MTUMISHI wa umma atakayeshindwa kuwasilisha cheti cha elimu na taaluma au “Index number” ya mtihani ili zihakikiwe na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), itakapofika Machi mosi mwaka huu, atakuwa kajiondoa kazini mwenyewe, imeelezwa.


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angellah Kairuki alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua Mkutano wa Watendaji Wakuu wa Wakala za Serikali jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

“Watendaji wakuu ninawaomba msimamie uhakiki wa vyeti ili watumishi wenu wafanye kazi kwa sifa stahiki,” alisisitiza Kairuki, katika taarifa iliyotolewa na wizara yake.

Aliongeza kwamba serikali ilisitisha ajira mpya ili kupisha kazi ya kuondoa watumishi hewa, ambayo imefika ukingoni na siku za karibuni, ajira zitarudishwa.

Akiwa mjini Dodoma, Septemba mwaka jana, wakati wa kuapishwa kwa wakurugenzi watendaji wapya 13 walioteuliwa Septemba 10, mwaka huu, Kairuki alisema kuanzia serikali imewaondoa watumishi hewa 17,201 kwenye utumishi wa umma na kazi hiyo inaendelea.

Kairuki aliwataka watendaji wakuu kuweka mikakati ya kuepuka watumishi hewa na kusimamia kwa dhati kwa sababu jambo hilo, limeumiza na kupoteza rasilimalifedha nyingi za serikali.

Alisema anatambua kuna wakala zenye upungufu wa watumishi, hivyo zinaingia gharama kubwa za kuajiri wafanyakazi wa mikataba, hata hivyo alielekeza kila Mtendaji Mkuu ajiridhishe kwa kuandaa taarifa ya mahitaji halisi ya watumishi.

Pamoja na hilo, Kairuki alielekeza wakala zenye watumishi wa mikataba zifanye tathmini na kuhakiki kama kweli watumishi hao wanahitajika kwa kuwa eneo hilo ni moja ya maeneo yenye ajira za mashaka kwa baadhi ya taasisi.

Aliongeza kuwa yapo malalamiko kuhusu suala la maadili na uwajibikaji yanayozigusa Wakala za Serikali.

Aliainisha masuala hayo ni pamoja na watumishi hewa, taarifa chafu za watumishi, matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma, kutosimamia ipasavyo utekelezaji wa mifumo ya utendaji kazi na wakati mwingine kutotekeleza majukumu ya msingi ya wakala.

Alifafanua kuwa amegundua kupitia taarifa mbalimbali kuwepo kwa changamoto ya mawasiliano hafifu kati ya wizara mama na wakala zilizo chini yao ambapo taarifa kutoka katika wakala hazichambuliwi inavyostahili na hata zinapochambuliwa na wizara mama, hazitoa mrejesho kwenda katika wakala.

Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Utumishi), Dk Laurean Ndumbaro alizitaka wakala za serikali kuimarisha eneo la ufuatiliaji na tathmini ili kuimarisha utendaji kazi na kuleta mabadiliko yanayotarajiwa na Watanzania.

Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post