ASKARI WAFICHUA UFISADI SARE ZA MAGEREZA



BAADA ya Rais John Magufuli kulipiga marufuku Jeshi la Magereza na majeshi mengine nchini kuruhusu askari wake kununua sare kwa watu binafsi, askari wa jeshi hilo wameibuka na kudai kuwa wamekuwa wanauziwa sare hizo kwa Sh 45,000.

Pia wamesema kofia na mikanda licha ya kuwa haiuzwi kwenye maduka ya watu binafsi, lakini upatikanaji wake pia ni wa shida, hali ambayo inawalazimu askari kutoa rushwa kwa wahifadhi bohari ili kupatiwa sare hizo.

Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti, askari mbalimbali waliohojiwa na gazeti hili licha ya kumpongeza Rais Magufuli kwa kulikemea suala hilo, walisema ni rahisi kushona kombati uraiani kwa kuwa vitambaa vinapatikana madukani, lakini kofia na mkanda ikichakaa askari analazimika kutoa pesa ili kupata mavazi hayo.

“Hizi kofia na mikanda inatolewa bohari ya jeshi, lakini kuupata huko mkanda au kofia lazima utoe rushwa kwa askari anayefanya kazi pale,” alisema mmoja wa askari aliyehojiwa na gazeti hili.

Wengi wa askari hao walisema kutokana na ugumu wa kupatikana na kofia na mikanda ya jeshi hilo, wengi wao wanaendelea kutumia kofia na mikanda waliyopewa wakati wanamaliza mafunzo.

Walisema kinachotolewa bure na jeshi hilo kwa sasa ni vyeo tu na sio sare nyingine yoyote. “Kofia hii ninayotumia pamoja na mkanda ni ile niliyopewa wakati namaliza depo (mafunzo) mwaka 2001,” alisema askari huyo ambaye ana miaka 15 sasa kazini na kuongeza, “Magereza wanachotoa bure kwa askari wao ni zile alama za cheo tu, vingine vyote vinavyohusu sare lazima askari ajinunulie.”

Wakati askari Magereza wanajinunulia sare, serikali imekuwa inatoa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwahudumia askari hao.

Mfano, katika bajeti ya mwaka 2015/16 serikali ilitoa Sh bilioni 167.1 kwa jeshi hilo.

Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 67.7 zilitolewa kwa jeshi hilo kwa ajili ya matumizi mengineyo, Sh bilioni 97.7 kama mishahara na fedha za maendeleo zilizotolewa kwa polisi ni Sh bilioni 1.6 Askari mmoja ambaye yuko mkoani Simiyu aliyefanya mahojiano na gazeti hili, alisema upatikanaji wa sare za Magereza kwa askari walioko mikoani ni mbaya, kwani wamekuwa wanalazimika kununua suruali na shati kati ya Sh 40,000 na 45,00 na viatu Sh 40,000.

“Juzi nilikuja hapo Dar es Salaam, nikawa na shida ya mkanda na kofia, nililazimika kutoa Sh 30,000 ambayo kofia niliinunua kwa Sh 10,000 na mkanda nilinunua kwa Sh 20,000,” alisema askari huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini. Alipoulizwa anazipataje sare za jeshi hilo, alifafanua, “Sisi ukitaka sare unaenda kwa fundi unachukuliwa vipimo vya shati na suruali, unamtumia askari mwenzako wa Dar es Salaam anakununulia kitambaa na kukushonea, kisha anakutumia.”

Alisema yeye tangu amalize mafunzo mwaka 2009 hajawahi kupewa sare yoyote. “Sijawahi kupewa mkanda, kofia wala viatu vyote tunajinunulia... mkanda nilio nao na kofia ambayo imeisha nilipewa wakati namaliza mafunzo, hadi juzi nilipokuja huko ndipo nikafanya jitihada za kupata kofia na mkanda mwingine,” alisema.

Askari mwingine wa kike anayefanya kazi jijini Dar es Salaam, alisema wamekuwa wanajinunulia vitambaa katika duka la Khimji na kwenda uraiani kushona sare hizo.

“Unachagua mwenyewe fundi wako, lakini mita ya kitambaa tunanunua kwa Sh 8,000 pale kwa Khimji, mashono yanategemea na fundi utakayempelekea mwenyewe,” alisema askari huyo na kuongeza kuwa wamekuwa wananunua soksi pia kwa Sh 4,000 huko uraiani.

Aliongeza kuwa yeye alimaliza mafunzo mwaka 2001 na tangu wakati huo amekuwa anavaa mkanda na kofia aliopewa akiwa mafunzoni.

“Sijawahi pata mgawo wowote wa sare tangu nitoke mafunzoni,” alieleza.

Alifafanua kuwa hata pale askari akihitaji kofia akienda kuomba bohari askari wanaofanya kazi kwenye hizo bohari wanataka wapewe rushwa ndipo waitoe.

“Hivi hivi huwezi pata kofia wala mkanda, lazima utoe kitu kidogo kwa anayefanya kazi bohari, kwa kweli mimi nilienda siku moja nikapata usumbufu sikuwahi tena kurudi huko,” aliongeza.

Kuhusu viatu, alisema wengi wa askari wanaofanya kazi Segerea na Ukonga wamekuwa wananunua viatu kwa mafundi wa uraiani ambao wanachonga viatu vinavyofanana na vya Magereza.

Alisema kwa sasa wananunua duka moja lililoko Mombasa, Ukonga ambako kuna huyo mtu anayevishona viatu vya aina hiyo. Askari mwingine wa kike alisema amekuwa anashona shati kwa Sh 10,000 uraiani na kwenye kiwanda cha Magereza anashona kwa Sh 5,000. Bei hiyo pia ni kwa sketi. Alisema sare kamili lazima igharimu mita 3.

“Pale dukani Kwa Khimji tunanunua kwa bei ya jumla ya shilingi elfu nane kwa meta, lakini ukienda maduka mengine ya rejareja unapigwa hadi shilingi elfu kumi na mbili kwa mita,” alibainisha.

Askari mwingine aliyeko mkoani Mwanza akizungumza na gazeti hili alisema wao kambini kwao walipatiwa mgawo wa mwisho mwaka 2012 na tangu wakati huo hawajapewa mgawo wowote.

Alisema wamekuwa wanaagiza sare Dar es Salaam kwa kutuma fedha Sh 40,000 au Sh 45,000 pamoja na vipimo, askari mwenzako anaenda kukununulia na kukutumia.

“Mimi hapa kofia yangu imetoboka, lakini kuipata kofia ni ngumu zaidi maana hizo hazipatikani kwingine kokote kama ilivyo kwa mkanda ambao nao unakaa nao miaka mingi hadi unabadilika rangi,”alisema askari huyo wa kiume.

Alisema mara nyingi wamekuwa wananunua viatu kwenye mitumba.

Alisema soksi pia wananunua zile zinazofanana na rangi ya magereza uraiani kwa Sh 5,000. Kutokana na jeshi la Magereza kutokuwa na utaratibu wa kuwagawia askari wake sare, wamekuwa hawana uwezo wa kudhibiti sare hizo kuvaliwa uraiani na kampuni zingine za ulinzi au hata mashule.

Kuna baadhi ya shule pia zimekuwa zinawashonea wanafunzi wao vitambaa hivyo vinavyotumiwa pia na askari wa magereza.

Mojawapo ya shule hizo ni Shule ya Sekondari ya Kitunda ambayo wanafunzi wanavaa sketi na suruali zinazofanana na sare ya Jeshi la Magereza. Kamishna Mkuu wa Magereza, John Minja alipotafutwa jana atoe ufafanuzi wa sababu ya askari wake kushona sare uraiani, simu yake iliita bila majibu.

Hata alipoandikiwa ujumbe mfupi wa maneno katika simu yake ya mkononi, alisema yuko kwenye kikao. Juzi Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza kwenye kambi ya jeshi la Magereza ya Ukonga na kueleza kuwa na taarifa za askari wa jeshi hilo kununua sare kwenye maduka ya watu binafsi.

Alipiga marufuku askari hao kuendelea kununua sare uraiani badala yake akataka jeshi hilo liwape bure hizo sare.

“Wakati wa utawala wangu askari wote wapate sare bure, wataenda kununua uraiani nikimali za muda wangu. Na kuanzia leo maduka yote ya raia yaliyoko kwenye kambi za kijeshi yaondolewe na wauza sare hizo wakome kufanya biashara hiyo mara moja,” alisema.

Alisema kuna baadhi ya maofisa wa jeshi hilo la Magereza wamekuwa wanashirikiana na watu binafsi kufanya biashara ikiwemo kuuza sare za jeshi, jambo ambalo alisema ni kinyume kabisa na taratibu za jeshi hilo.

CHANZO-HABARILEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post