UKWELI HALI MBAYA ZA BENKI TANZANIA WAANIKWA


Msajili wa Hazina nchini, Lawrence Mafuru amesema benki nchini zinashindwa kueleza ukweli juu ya kuyumba kwao na kwamba madai ya kuwa hali zao ni mbaya kutokana na agizo la serikali la kutaka fedha zake zitunzwe Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hazina ukweli.

Mafuru amesema taarifa ambazo serikali wanazo ni kwamba benki hizo zaidi ya 50 zimekopesha fedha nyingi kwa watu mbalimbali, lakini marejesho ya madeni hayo yamekwama kiasi cha kusababisha benki hizo ziwe katika hali hiyo.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Msajili wa Hazina licha ya kukiri kuwa mzunguko wa fedha umepungua kutokana na Tanzania kuchagua kwamba fedha inazozipata zitumike katika miradi ya maendeleo badala ya matumizi ya kawaida, benki zinazolalamika zimeshindwa kurejesha fedha ilizokopesha watu na taasisi mbalimbali.

Akizungumzia taarifa zinazoenezwa kwamba benki zimekosa fedha za kujiendesha, Mafuru alisema taarifa walizozipata ni kwamba Septemba mwaka huu, benki hizo zaidi ya 50 nchini zimekopesha zaidi ya Sh trilioni 16.3 kwa watu mbalimbali.

Hata hivyo, alisema kati ya fedha hizo, Sh trilioni 1.43 zimekopeshwa bila ya kurudishwa katika benki husika na kwamba benki hizo zinashindwa kueleza ukweli uliopo badala yake wanalalamika kwamba hatua ya serikali kuamua fedha zake zitunzwe BoT badala ya katika benki za kibiashara, ndio sababu ya hali yao (benki) mbaya.

Kwa mujibu wa Mafuru, serikali imeamua kuchukua uamuzi huo wa kuzitoa fedha zake kutoka katika benki mbalimbali za kibiashara nchini kwa ajili ya kuwezesha serikali kujua mapato wanayopata kutoka katika taasisi zake.

Msajili wa Hazina amesema zaidi ya Sh bilioni 515 zimeingizwa BoT baada ya uamuzi huo wa Serikali ya Awamu ya Tano ambao ulitangazwa na Rais John Magufuli baada ya kushika madaraka mwaka mmoja sasa. Mafuru alikiri kuwa ni kweli kwamba mzunguko wa fedha umekuwa mdogo na kueleza kuwa chanzo chake si kwamba benki zimekosa fedha kwa ajili ya kujiendesha.

Alifafanua kuwa awali watu wengi walitegemea safari na posho ambazo baada ya chenji kubaki, walikuwa wakitumia bila ya malengo, lakini sio kwamba mzunguko huo wa fedha unawaathiri watu wote.

“Tumeona tusitegemee wahisani badala yake tujiwekeze katika miradi mikubwa ya maendeleo ambayo kwa sasa haitaonekana, lakini baadaye itasaidia kuondoa nafasi iliyopo sasa,’’ alisema Mafuru.

“Tayari shilingi bilioni 515 zimeingizwa BoT na mpaka Septemba mwaka huu fedha hizo zilikuwa kwenye akaunti hiyo. BoT ni sehemu ya mfumo wa benki, kwani itakuwa inafanya kazi ya kukopesha kama zilivyo benki nyingine,” alifafanua Mafuru ambaye ofisi yake inasimamia mashirika na taasisi za umma.

Alifafanua kuwa ofisi yake ambayo ina jukumu la kusimamia mapato na matumizi, awali walikuwa wanapata shida kupata taarifa za mapato na matumizi katika benki hizo zilizopo kila kona nchini na kwamba baada ya BoT kuchukua dhamana hiyo, imewasaidia, kwani wanaandika barua na kupatiwa taarifa hizo kwa muda mfupi.

Alisema serikali inategemea mapato yake kutoka katika makundi matatu ambayo ni Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na kupitia mashirika na taasisi mbalimbali.

Alisisitiza kuwa itasaidia kujua mashirika hayo zaidi ya 260 namna wanavyotumia fedha zake katika miradi mbalimbali na kwamba suala la kuchukua fedha bila ya kuzitumia lisiwepo.

IMEANDIKWA NA FRANCISCA EMMANUEL- HABARILEO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post