RAIS MAGUFULI AGOMA KUFUKUA MAKABURI,ADAI YANAWEZA KUMSHINDA KUYAFUKIA

RAIS Dk. John Magufuli amezungumzia safari yake ya mwaka mmoja wa urais Ikulu, akieleza mafanikio na changamoto alizozikuta huku akisema kuna makaburi amelazimika kutoyafukua kwa sababu yanaweza kumshinda kuyafukia.

Ingawa hakufafanua juu ya makaburi hayo, kauli hii ya sasa inaelezwa kutoa taswira nyingine mpya ya Rais Magufuli ambaye tangu aingie madarakani amejipambanua kama mtu aliyekuja kusafisha nchi.

Kauli hiyo aliitoa jana katika mkutano wake na wahariri pamoja na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kurushwa moja kwa moja na televisheni na redio.

Rais Magufuli alilazimika kutoa kauli hiyo wakati akijibu swali aliloulizwa na mmoja wa waandishi waliohudhuria mkutano huo aliyetaka kufahamu changamoto alizozikuta katika nafasi aliyoishikilia sasa.

“ Nimeshughulikia changamoto mbalimbali lakini siwezi kuyafukuwa makaburi yote kwa sababu kuna mengine nitashindwa kuyafunika, sikuja kufukua makaburi nataka kuanza na yale niliyoyakuta ili tujenge Tanzania yetu,” alisema.

Katika hilo alisema kazi ya kuiongoza nchi sio nyepesi na hivyo kuwashangaa wale wanaoutaka urais.

“ Nilibeep, ikaita ikajipokea, kazi ya urais sio nyepesi, wanaotaka urais nawakaribisha sana,” alisema Rais Magufuli.
Katika kuonyesha ugumu wa kazi hiyo, Rais Magufuli alisema wakati mwingine analazimika kulala usiku wa manane.

“Nalala saa tisa au saa kumi usiku wakati mwingine” alisema .
Alikwenda mbali na kusema kazi ya kuijenga Tanzania asiachiwe Rais peke yake hivyo akawataka waandishi wa habari kuhakikisha wanamsaidia katika kufichua maovu yanayotendeka serikalini.

“Rais hawezi kuona kila kitu lakini ninyi mna jukumu la kuhakikisha mnafichua maovu na mimi ninasoma kila kitu mnachoandika na mengine nikiyafuatilia nakuta yana ukweli ndani yake ,” alisema.

KATIBA MPYA
Rais Magufuli pia alizungumzia mchakato uliokwama wa upatikanaji wa Katiba Mpya akisema aachwe anyooshe nchi kwanza.

Licha ya kusema kwamba mchakato huo ulikuwa umefika katika hatua nzuri lakini yeye binafsi suala la Katiba hakupata kulizungumzia katika kampeni zake.

“Tutengeneze nchi kwanza, nimezunguka nchi nzima wakati wa kampeni sikuzungumzia Katiba Mpya  kwa hiyo katiba zinaweza kuwa nyingi tu lakini kwa sasa mniachw ninyooshe nchi kwanza,” alisema Rais Magufuli.

MADUDU MAPYA
Akielezea changamoto alizozikuta ikiwamo ile ya mtandao wa wizi wa fedha za umma Rais Magufuli alifichua jinsi fedha za serikali zilivyokuwa zinatafunwa na wapiga dili kupitia mgongo wa benki  mbalimbali hapa nchini.

Alisema baadhi ya wakurugenzi wa mashirika ya Umma walikuwa wanachukuwa fedha za serikali na kuzipeleka benki kwa mtindo wa kuzihifadhi kwa njia ya ‘fixed account’ na kisha kuzitumia kufanya biashara na serikali.

“ Nimekata mirija ya wapiga dili wote, Tanzania inabenki zaidi ya 50, zote hizi zilimuhudumia mwananchi kwa asilimia 20, kiasi kilichobaki eti walitegemea kufanya biashara na Serikali.

“ Haiwezekani baadhi ya wakurugenzi walikuwa wanachukua fedha za umma wanapiga dili na watu wa benki kwa kuziweka fedha hizo kwenye ‘fixed account’ halafu benki hiyo inazitumia kuikopesha Serikali tena kwa asilimia 16, nimekata mirija hiyo na hao wapiga dili waendelee kulia kuzikosa hivyo hivyo hizo fedha,” alisema.

Alisema mbali na wakurugenzi pia baadhi ya wanasiasa walitumia mashirika ya umma na benki hizo kuchota fedha za umma.

Alilitaja Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuwa ni miongoni mwa mashirika ya umma yaliyotumiwa na wanasiasa kujichotea fedha.

“Unamuona mtu anapiga kelele wee, unadhani yuko clean( safi) lakini unakuta majina yao yapo kwenye madeni… wanakwenda kukopa mabilioni ya fedha tena bila kulipa, wengine kumbe walikuwa wanaishi bure katika nyumba za mashirika ya umma bila kulipa kodi lakini ndio wapiga kelele wakubwa.

“Yalikuwa yakifanyika mambo ya ovyo ovyo tu ya dili, hata ndani ya CCM wapo watu wa ovyo ovyo wapiga dili, nataka  niwaambie bila kufanya kazi hawataiba hata senti tano,”.
Akizungumzia mtazamo wa watu wanaomuona kuwa anatumia hoja ya maendeleo kuminya demokrasia, Rais Magufuli alipuuza hoja hizo.

“ Hivi karibuni mmesikia chama kimoja cha kisiasa kwenye vikao vyao vya ndani wanagombana wao kwa wao sasa hiyo demokrasia naiminya vipi?. Mmeona chaguzi zinaendelea hata hapa wamechagua Ukawa, Lakini pia tunatakiwa kujua demokrasia ina mipaka yake baada ya uchaguzi watu waendelee na uzalishaji”.

BARAZA LA MAWAZIRI

Katika kuelezea mafanikio ya mwaka wake mmoja wa urais madarakani, Rais Magufuli licha kusema zipo changamoto katika Baraza lake la Mawaziri lakini alisema bado ana imani nalo.

“Serikali niliyounda imenisaidia sana na wanafanya kazi zao vizuri, niliona niwe na baraza la watu wachache  katika kuwatumikia wananchi,” alisema.

Akizungumzia suala la huduma za afya hususani  changamoto ya kukosekana dawa, alisema katika bajeti ya mwaka 2016/17  Serikali yake ilitenga sh. bilioni 1.99 kwa ajili kununua dawa.

“Tumebadilisha utaratibu badala ya kununua dawa kutoka kwa wasambazaji sasa tunanunua moja kwa moja kutoka viwandani pia kuna nchi zinataka kuwekeza hapa nchini kwa kujenga viwanda vya kutengeneza madawa,” alisema Rais.

Alizungumzia suala la uchumi wa viwanda  alisema Watanzania wasiitegemee Serikali katika kujenga viwanda na kwamba inachofanya ni kuhamashisha watu binafsi kuwekeza katika eneo hilo.

Pamoja na hilo Rais Magufuli alisema serikali yake imetimiza lengo lake la makusanyo ya kodi yanayofikia sh. trilioni 1.2 kutoka sh. bilioni 800.

Alisema katika bajeti ya  fedha ya mwaka 2016/17 serikali yake imetenga asilimia 40 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, huku ikiwa tayari imenunua  ndege mbili aina ya Bombardier Dash 8 Q400.

Kwa mujibu wa Rais Maguli serikali yake inatarajia ndege nyingine mbili aina ya Jeti pamoja na Bombardier na mwaka 2018 ataongeza ndege aina ya Boeing na kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano serikali itakuwa na jumla ya ndege saba.

Pamoja na hilo Rais Magufuli alielezwa kufurashwa na kasi ya kukuwa kwa uchumi kutoka asilimia 7 hadi kufikia asilimia 7.2 sasa.

Alisema kasi hiyo inaifanya Tanzania kuwa nchi ya pili barania Afrika nyuma ya Ivory Coast ambao kasi ya uchumi wake inakuwa kwa kasi.

AKWEPA SAFARI 47
Akifafanua dhana ya kubana matumizi, Rais Magufuli alisema kwamba alianza kwa kujibana mwenyewe ambapo alialikwa safari 47 lakini amekwenda safari tatu tu.
Alisema safari nyingine aliwakirishwa na mabalozi, Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri Mkuu pamoja na Makamu wa Rais.

“ Unajua  kusafiri kwangu lazima niwe na watu zaidi ya 40 lakini nikiwatuma wengine msafara wao huwa ni wa watu wawili kwa hiyo fedha nyingi inapona na tunaipeleka kwenye miradi ya maendeleo,” alisema Rais.

WAFANYABIASHARA
Kuhusu hoja ya serikali kuwatenga wafanyabiashara, Rais Magufuli alisema serikali yake haijawatenga na kwamba inawahitaji sana  na yeye anawapenda lakini anataka walipe kodi.

“Palikuwa na mambo ya ovyo, sitaki kwenda  kwenye details sana maana mambo mengine yapo  mahakamani ila niwaambie ukweli wafanyabiashara matapeli siwapendi”.

Akifafanua madai kupanda kwa mishahara licha ya wafanyakazi hewa kuondolewa Rais Magufuli alisema hilo limetokana na madai ya siku za nyuma ya wafanyakazi ambayo yamesababisha serikali yake kulipa sh. bilioni 22.6 huku kukiwa bado kukiwa na mengine 39,000 yenye thamani ya sh. Bilioni 23.

Alisema madai hayo mengi yalitokana na watu waliopandishwa vyeo kutolipwa fedha zao za kiwango cha nafasi waliyopewa, pia madeni ya watumishi kwenye mifuko ya jamii ambazo serikali ilikuwa bado haijawasilisha.

“Ndio maana nilisitisha ajira kwa miezi miwili, kwanza wakati huo kulikuwa na vijana wako mafunzoni jeshini nilisubiri wamalize mafunzo yao ili wakiingia kwenye ajira mpya tunaanza pamoja. serikali imeanza kutoa ajira na hadi leo imeajiri watumishi 5000, wamo madaktari 100 na tunataraji kuongeza 200 wengine katika hospitali yetu ya Mloganzila,” alisema.

MAPAMBANO YA UJANGILI/RUSHWA
Kuhusu mapambano dhidi ya ujangili  Rais Magufuli alisema Serikali yake imejipanga kuhakikisha inakomesha suala hilo.
Akizungumzia suala la mapambano dhidi ya Rushwa na Ufisadi, alisema matunda kuhusu yameanza kuonekana baada ya nidhamu kurejea makazini.

“ Tumepitisha sheria ya mafisadi  na sheria ilivyofika kwangu nilisaini siku hiyo hiyo, na kesi ya kwanza imeanza kusikilizwa jana (juzi). Rushwa ni  suala myambuka na haliwezi kushughulikiwa na Rais peke yake . Nitoe wito kwa Watanzania wote tukatae kwa sababu ni kansa ya maendeleo,” alisema.
Chanzo-Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post