BODI YA MIKOPO YAAGIZWA KULIPA POSHO ZA WANAFUNZI WANAOENDELEA NA MASOMO LEO JUMAMOSI




Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), imeagizwa kuhakikisha kuwa fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo zinapelekwa vyuoni ifikapo leo.


Agizo hilo lilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako baada ya wabunge mbalimbali kuomba miongozo kwa Spika kuhusu kuwapo kwa wanafunzi wengi waliokosa mikopo kwa mwaka wa fedha 2016/17.


Mwongozo kwa Spika ulitiliwa mkazo na Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwan Kikwete aliyeeleza kuwapo taarifa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuwa wanafunzi wanataka kugoma kwa kukosa fedha za mikopo.


Kutokana na miongozo hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga aliitaka Serikali kutoa maelezo.


Akitoa kauli ya Serikali, Profesa Ndalichako alisema fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi zilikwenda vyuoni wiki moja iliyopita.


“Tatizo lililotokea kwa UDSM sijui kama walidanganyana au la lakini hawakujaza fomu. Serikali haitatoa mkopo kwa mwanafunzi ambaye hajajaza fomu. Na waliosaini leo wataingiziwa fedha zao kwenye akaunti na vyuo,”alisema.


Kuhusu wanaoendelea na masomo, Profesa Ndalichako alisema wanafunzi wote wanufaika na wanaoendelea na masomo wataendelea kupatiwa mikopo kama ilivyokuwa mwaka uliopita.


Alisema wanafunzi ambao vyuo vyao vimewasilisha HELSB taarifa za matokeo, Bodi imekwishawatumia fedha vyuoni kwa ajili ya kuwapa mikopo wanafunzi hao.

Hata hivyo, alisema taratibu za kuwabaini wanafunzi wenye sifa zinaendelea na wasio na sifa wataendelea kuondolewa kupata mikopo.


Pia, alikiri kuwa ucheleweshaji wa matokeo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo umeathiri kasi ya kutuma fedha vyuoni.


“Wizara yangu imekwishaagiza vyuo vyote ambavyo havijawasilisha matokeo ya mitihani ya wanafunzi wao kwa mwaka wa masomo uliopita, kufanya hivyo mara moja,”alisema.


Ndalichako alisema hadi kufikia Novemba 3 mwaka huu, Sh71.042 bilioni zilikwishatumwa vyuoni kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo.


Akizungumzia utoaji wa mikopo kwa mwaka wa fedha 2016/17, Ndalichako alisema katika mwaka huo, Sh483 bilioni zimetengwa na zimelenga kutoa mikopo kwa wanafunzi 119,012, wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo na wa mwaka wa kwanza 25,717.

Ndalichako alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 wanafunzi 58,010 walidahiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na orodha yao iliwasilishwa HELSB na hadi Novemba 2, mwaka huu, wanafunzi 21,190 wa mwaka wa kwanza wamepewa fedha. Kati yao 4,321 ni yatima, 118 wenye ulemavu na 87 ni waliosoma sekondari kwa ufadhili wa taasisi mbalimbali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post