Picha: MAZISHI YA MAREHEMU JOSEPH MUNGAI MJINI MAFINGA MKOANI IRINGA


Familia ya Marehemu Joseph Mungai ikiwa imeshikana mkono ishara ya upendo wakati wa mazishi ya baba yao mjini Mafinga wilaya ya Mufindi mkoa wa Iringa.

Baadhi ya waombolezaji wakiwa katika mazishi ya Mzee Joseph Mungai huko Mafinga wilaya ya Mufindi mkoa wa Iringa.

Waziri mkuu mstaafu Mhe. Frederick Sumaye akitoa salama zake kwa niaba ya mwenyekiti wa Taifa wa Chadema katika mazishi ya Mzee Joseph Mungai huko Mafinga wilaya ya Mufindi mkoa wa Iringa.

Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu na waombolezaji wengine wakitoa heshima za mwisho katika mazishi ya Mzee Joseph Mungai huko Mafinga wilaya ya Mufindi mkoa wa Iringa.

Mbunge wa Mikumi Mhe. Joseph Haule akitoa heshima zake za mwisho

Waziri wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya makazi Mhe. Wiliam Lukuvi akiteta jambo na mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu wakati wa mazishi ya marehemu Mungai.

*****

WAZIRI wa Ardhi Nyumba na maendeleo ya makazi ,Wiliam Lukuvi aongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa waziri wa Elimu na mbunge wa mstaafu wa jimbo la Mufindi kaskazin Joseph Mungai.

Akizungumza katika ibada ya mazishi leo  mjini Mafinga wilaya ya Mufindi Lukuvi ambae alimwakilisha Rais Dkt John Magufuli alisema kuwa Mungai atakumbukwa kwa uongozi wake uliotukuka hasa katika misingi mizuri ya elimu wa Elimu ya Sekondari (MMES).

Lukuvi alisema kuwa wakati serikali ilipoanzisha suala la Sekondari za Kata, Mafinga na Mufindi kwa ujumla mwamko huo ulishaanza toka miaka ya 1980 ambayo kwa uongozi wake kama Mbunge alihamasisha Wananchi kutoa michango, kufyatua matofalina kina mama kuchota maji yote hiyo nji katika kufanikisha adhima ya kusogeza elimu ya sekondari kwa watu wengi.

“Alianza kuwa kiongozi akiwa na umri mdogo kuliko wanasiasa wote wa Mkoa wa Iringa wakati huo, lakini pia alikuwa kiunganishi pale kunapotokea misuguano yoyote hakuwa na makuu na kama ulikuwa ukitaka ushauri basi utaupata kwa mzee wetu mungai ,” alisema.

Akiongoza ibada ya mazishi askofu wa KKKT dayosisi ya Iringa Dkt Owdenburg Mdegella alisema kuwa kila mwanadamu aishie chini ya hili jua anapaswa kuishi maisha ya kumuabudu mungu na kuachana na tabia ya kuhukumiana hapa duniani kwakuwa kila mtu atajibu dhambi zake akiwa mbinguni.

Dkt Mdegela alisema Mungai ni moja kati ya viongozi wachache waioacha historia kubwa hapa nchini kutokana na uongozi wake uliotukuka wa kupigania maendeleo ya watanzania bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

“Leo tumempoteza mtu muhimu sana ndugu yangu Lukuvi...mimi na wewe tunapaswa kukaa chini na kuangalia mustakabali wa mkoa wetu wa Iringa. Ameondoka mzee Peter Siyovvela ameondoka Adam Sapi na leo ameondoka mzee wetu Mungai sasa ni wakati wetu kwani kwa Iringa tumebaki mimi na wewe sasa tukutane kabla mwaka haujaisha ili kujadili jambo hili alisema” Mdegella


SUMAYE
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema Waziri Mkuu mstaafu Mhe. Fredrick Sumaye alisema kuwa Taifa la Tanzania kimepoteza kiongozi makini aliyekuwa na uthubutu wa kutenda mambo bila ya ubaguzi na kusimamia kile anacho kiamini katika kuwatumikia watanzania.

Alisema kuwa Mungai alikuwa ni mtu mchapakazi aliyekuwa na hoja alizozijenga na kuzisimamia kikamilifu kwani alitamani sana kutenda mambo kwa haki bila ya kubaguana kiitikadi bali alisimama katika haki.

Alisema kuwa chama cha demokrasia na maendeleo chadema kimesikitiswa sana na kifo chake kwani alikuwa ni mtu mpenda demokrasia hivyo katika muuenzi na kutambua mchango wake Hapa nchini watanendeleza kudumisha misingi mizuri ya demokrasia aliyokuwa akiishi marehemu Mungai 


Luhavi
Kwa upande wake Naibu Katibu mkuu wa chama cha mapinduzi Rajabu Luhavi alisema Mungai atakumbukwa kwa uongozi wake uliotukuka kwa wa kuwatumikia watanzania bila ya ubaguzi.

“Alikuwa kiongozi mzuri tangu uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Ametoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu. Tunapaswa kuenzi yale mazuri waliyoyafanya na sisi tunaanzia pale alipoishia.

Akizungumza wasifu wa marehemu Denis Mungai alisema kuwa Mungai aliwahi kuwa Mbunge wa Mufindi kupitia CCM kwa miaka 35.

Pia amewahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini enzi za utawala wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na pia katika awamu za pili, tatu na nne.

Baadhi ya nyadhifa alizowahi kushika kwa nyakati tofauti ni uwaziri wa iliyokuwa Wizara ya Elimu na Utamaduni, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Wabunge
Baadhi ya wabunge wa majimbo ya Mkoa wa Iringa wakizungumzia Mungai huku kila mmoja akisema alikuwa kiongozi mkweli aliyesimamia alilokuwa analiamini.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema Mungai alikuwa kiongozi wa wazi asiyegopa kusimamia ukweli.

Alisema amepokea kwa mshtuko taarifa ya msiba huo na kubainisha kuwa alimfahamu Mungai akiwa nje ya ulingo wa siasa.
“Alikuwa kiongozi mzuri tangu uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Ametoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi yetu, tunapaswa kuenzi yale mazuri waliyoyafanya na sisi tunaanzia pale alipoishia.

“Alikuwa kiongozi muwazi na alituunga mkono wapinzani ingawa hakushinda… kwa ujumla alikuwa mtu mkweli asiyefungamana na siasa za upande wowote,” alisema Msigwa.

Mbunge wa Mafinga mjini Cosato Chumi alisema kuwa watu wa Mafinga na Mufindi kwa ujumla wamempoteza mtu muhimu sana kwani atakumbukwa kwa mengi aliyofanya hasa mwamko na kuisogeza elimu ya sekondari kwa watu wa kawaida kupitia Mufindi Education Trust-MET.

Chumi alisema kuwa wakati serikali ilipoanzisha suala la Sekondari za Kata, Mafinga na Mufindi kwa ujumla mwamko huo ulishaanza toka miaka ya 1980 ambayo kwa uongozi wake kama Mbunge alihamasisha Wananchi kutoa michango, kufyatua matofali na kina mama kuchota maji katika kufanikisha azma ya kusogeza elimu ya sekondari kwa watu wengi.

“Kwa jitihada zake mzee Mungai Mufindi ndio Wilaya ya Kwanza hapa nchini kuwa na Bank ya Wananchi yaani Community Bank (Mucoba) ambayo imeendelea kuwa kimbilio la tabaka la chini na Kati katika suala zima la mikopo na huduma za kibenki.

"Mimi nawaombea faraja wanafamilia wote katika kipindi hiki cha majonzi. Mungu ailaze Roho yake Mahali Pema Peponi - Amina alisema Chumi ”.

Picha na Habari kwa hisani ya MatukiodaimaBlog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post