MTANZANIA ATUNUKIWA TUZO YA HESHIMA NA PAPA FRANCIS


Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Baba Mtakatifu Fransisko

****
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Fransisko amemtunuku tuzo ya heshima aliyekuwa mkuu wa Idara ya afya mstaafu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Daktari Fredrick Kigadye kutokana na mchango mkubwa alioutoa kwa kanisa Katoliki.

Mwadhama, Askofu Mkuu Polycarp Kardinali Pengo wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Fransisko alikabidhi tuzo hiyo kwa daktari Kigadye jijini Dar es Salaam katika hafla fupi iliyofanyika baraza la maaskofu. Baada ya kukabidhi tuzo hiyo Kardinali Pengo alisema amejisikia furaha kwa tendo hilo kubwa katika kanisa lao hapa nchini la daktari Kigadye kupewa tuzo hiyo.

“Daktari Kigadye ametusaidia sana katika masuala ya Pasada kwa hiyo nina sababu ya ziada ya yale yaliyoongelewa ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa tukio hili. Ni shukrani kubwa kwa Baba Mtakatifu Fransisko aliyeridhia ombi la maaskofu kutoa hii hati pamoja na nishani.Hati ikitolewa na Mwenyezi Mungu mambo mengine ni ziada,” alisema Pengo.

Naye daktari Kigadye alitoa shukrani zake kwa Mungu, Baba Mtakatifu Fransisko na kwa maaskofu wote waliochangia jambo hilo kufanikiwa.

“Asante kwa Mwenyezi Mungu kwa uhai na majaliwa yote kwangu na wote walioshiriki katika malezi yangu hadi kufikia siku ya leo kihistoria,” alisema daktari Kigadye.

Kwa upande wake rais wa Maaskofu Katoliki Tanzania, Tarcisius Ngalalekumtwa alimtaka daktari huyo asijisifu wala kujivuna kwa kuwa jambo hilo lililofanyika ni kazi ya Mungu.

Tuzo hiyo ‘Bene Merenti’ maana yake ikiwa ni ‘kwa yule anayestahili’ ilipokelewa kwa furaha na katibu mkuu wa TEC, Padri Raymond Saba.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post