MAKUNDI ya mbwa wanaokadiriwa kufikia 100 yamezua taharuki kubwa kwa wafugaji katika Wilaya ya Kalambo na Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa ambao wanadaiwa wameshaua mbuzi 120, kondoo 12 na ndama sita katika kipindi cha miezi mitatu sasa.
Mbwa hao wanaoishi porini wamezua taharuki katika vijiji vya Katazi na Ninga wilayani Kalambo na kijiji Kankwale katika Manispaa ya Sumbawanga.
Akizungumza na gazeti hili, Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Julieth Binyura amekiri kuwepo kwa mbwa hao katika vijiji vya Katazi na Ninga akisisitiza mbwa hao wanadaiwa walitelekezwa na mganga wa kienyeji aliyekuwa akiishi katika Kijiji cha Ninga.
Alidai kuwa simulizi zilizopo ni kwamba mganga huyo wa kienyeji alihamia kijiji kingine na kufikwa na umauti ambapo mbwa wake walihamia porini na kuzaliana.
“Tayari nimemwagiza ofisa mifugo awaue mbwa hao, lakini ameweza kumuua mmoja tu ikidaiwa kuwa mbwa hao wapo wengi, lakini wanapowindwa anaonekana mbwa mmoja tu…. Ni kwamba mbwa hawa wakimkamata mnyama hasa mbuzi huvunja shingo na kunywa damu yake huku wakiacha mizoga ya wanyama hao,” alieleza.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ninga, Yohana Kawea amedai kuwa idadi ya mbwa hao wanakadiriwa kuwa zaidi ya 100 ambapo tayari wameua mbuzi 80 na ndama mmoja kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
“Mbwa hawa walikuwa wanamilikiwa na mganga wa kienyeji aliyekuwa akiishi kijijini hapa lakini alipohamia kijiji Chalatila aliwaacha hivyo wakahamia porini na milimani na wamezaana sana, kwa sasa wanafika mbwa mia moja kwa idadi... “Wanatishia amani wafugaji awali walikuwa wakiua mbuzi wanakula nyama yake yote, lakini sasa wakiua wananyonya damu tu kisha wanaacha mzoga ….wanaweza kuua mbuzi kumi kwa siku hivyo wafugaji huuza nyama ya mizoga hiyo kwa wananchi huku wengine wakipika na kwenda kuuza kwenye vilabu vya pombe za kienyeji,” alisema.
IMEANDIKWA NA PETI SIYAME,HABARILEO KALAMBO