Kimenuka!! AJALI YA NOAH,LORI ILIYOUA 19 SHINYANGA YANG’OA VIGOGO WA POLISI....WATUMBULIWA


Jeshi la polisi nchini kupitia kikosi cha usalama barabarani limewavua nyadhifa zao mkuu wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Tabora (RTO) Shida Machumu, na mkuu wa usalama barabarani wa wilaya ya Nzega (DTO) Thomas Sengecha kwa kushindwa kuwasimamia askari wa usalama barabarani na kusababisha kutokea kwa ajali ya Noah na lori iliyoua watu 19 na kujeruhi wawili mkoani Shinyanga.

Uamuzi huo umetolewa leo November 09,2016  na Kaimu kamanda wa kikosi cha usalama barabarani Tanzania SACP Fortunatus Muslimu wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari mkoa wa Shinyanga kuhusu hatua zilizochukuliwa na jeshi la polisi baada ya kutokea kwa ajali hiyo.

Ajali hiyo iliyoua watu 19 na kujeruhi watu wawili ilitokea Novemba 6,2016 katika kijiji cha Nsalala wilaya ya Shinyanga baada ya gari T232 BQR aina ya Toyota Noah iliyokuwa inatoka Nzega mkoani Tabora kwenda Tinde mkoani Shinyanga kugongana na lori aina ya Scania lenye namba T198 CBQ likiwa na tela namba T283 CBG likitoka Tinde kwenda Nzega.

Muslimu alisema viongozi hao wanaondolewa katika nyadhifa zao kwa kushindwa kuwasimamia askari wa usalama barabarani ambao walioondoka katika vituo vyao vya kazi na kusababisha Noah kubeba abiria 21 badala ya abiria wanane kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria.

Kamanda Muslimu alisema baada ya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu ajali hiyo wamebaini kuwa inatokana na uzembe uliofanywa na askari waliokuwa zamu kwenye kituo cha mabasi cha Nzega ambao waliondoka kituoni na kusababisha gari aina ya Noah kubeba abiria 17,kati yao watu wazima 13 na watoto wane waliokuwa wamepakatwa na wazazi wao.

“Gari aina ya Noah ilianza safari katika kituo cha Nzega ikiwa na abiria 17 majira ya saa 12:30 jioni...wakati gari linaondoka askari waliopangwa kazini eneo hilo walikuwa wameshaondoka kituoni hivyo gari hilo halikukaguliwa hivyo kutoa mwanya kwa gari hilo kubeba abiria kupita kiasi kwa kuzidisha abiria”,alieleza Muslimu.

Alisema kitendo cha askari kuondoka eneo la tukio,kilifanya gari izidishe abiria watano watu wazima na watoto wanne kwani Noah inapaswa kubeba abiri wanane na si vinginevyo kwa mujibu wa sheria.

Aliongeza kuwa vile vile askari waliopangwa kazini barabarani eneo la Uchama- Nzega nao walikuwa wameondoka eneo hilo hivyo kutoa mwanya mwingine wa gari hilo kubeba abiria wengine wanne njiani eneo la Nata ambapo inadaiwa kulikuwa na basi lilikuwa limeharibika na abiria kusimamisha Noah.

“Noah ilisimama na abiria kulazimisha kupanda ndani ya gari hilo na hivyo kuongeza idadi ya abiria katika gari hilo kufikia jumla ya watu 21 pamoja na dereva na hivyo ndani ya Noah kuwa na watu 22 na dereva akaendesha gari kwa mwendo kasi bila kuchukua tahadhali na kasha kugongana na lori”,alieleza Muslimu.

Alisema ajali hiyo imechangiwa na uzembe uliofanywa na askari kwa kuondoka eneo la kituo cha Mabasi Nzega na barabarani kituo cha Buchama hivyo mkuu wa usalama barabarani wa mkoa wa Tabora pamoja na wilaya ya Nzega wanaondolewa katika nyadhifa zao kwa kushindwa kusimamia askari hao.

“Tunamwondoa mkuu wa usalama barabarani wa wilaya ya Nzega Thomas Sengecha na mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Tabora Shida Machumu kwa kushindwa kutekeleza mkakati wa kupunguza ajali na kushindwa kusimamia na kuchukua hatua kwa watendaji walio chini yao kutokana na uzembe waliofanya”,alifafanua.

Muslimu alisema wakuu hao mbali na kuvuliwa nyadhifa zao pia wanaondolewa katika kikosi cha usalama barabarani na watapangiwa kazi nyingine na kwamba dereva wa Noah Seif Hemed (32) mkazi wa Tinde amefikishwa mahakamani na leseni yake tayari imeshafungiwa hataendesha tena gari.

Aidha askari wanne waliopangwa katika kituo cha mabasi cha Nzega ambao ni SGT Charles,E.6547 CPL Kheri,WP 6983 PC Happy na WP 7676 PC Neema na wawili kituo cha Buchama,WP 5791 PC Cecy na WP 7165 PC Aziza watachukulia hatua za kinidhamu na wanaondolewa moja kwa moja katika kikosi cha usalama barabarani.


“Hatuwezi kuendelea kuona ajali zinaendelea kutokea na kupoteza maisha ya watu kutoka na uzembe wa watendaji katika maeneo yao,hatutaki ajali tunataka tuishi salama,”alisema Muslimu.

Aliwataka askari na viongozi kuacha kufanya kazi kwa mazoea watekeleze majukumu yao ipaswavyo katika kuzuia ajali za abiria barabarani na kwamba wataendelea kuchukua hatua zinazostahili kwa askari wazembe na kuwawajibisha viongozi wote watakaoshindwa kutekeleza na kusimamia majukumu yao.

Na Kadama Malunde- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post