HAYA HAPA MAJINA YA WATU WALIOFARIKI KATIKA AJALI YA NOAH,LORI ILIYOUA WATU 18 SHINYANGA


Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro akiwa eneo la tukio-Tazama picha zaidi <<HAPA>>

******Watu 18 wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa baada ya gari lenye namba za usajili T 232 BQR Toyota Noah waliyokuwa wanasafiria kutoka Nzega mkaoni Tabora kuelekea Tinde kugongana uso kwa uso na lori aina ya Scania lenye namba za usajili T198 CBQ /T283 CBG) katika kijiji cha Nsalala kata ya Tinde wilaya na mkoa wa Shinyanga.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo,ajali hiyo imetokea Siku ya Jumapili Novemba 06,2016 saa moja na nusu usiku katika barabara ya Nzega- Tinde mkoani Shinyanga.

Wakizungumza na Malunde1 blog mashuhuda wa ajali hiyo walisema dereva wa gari aina ya Noah alikuwa anajaribu kuyapita magari mengine yaliyokuwa mbele yake na ghafla akagongana na lori hilo na kusababisha vifo vya watu 15 papo hapo.

“Ni ajali ya kutisha,watu 15 wamepoteza maisha papo hapo waliokuwa kwenye Noah ambayo ilikuwa imejaza watu wengi,watu wengine watatu wamefariki wakati wakipelekwa hospitali kupatiwa matibabu”,alieleza Mohammed Ali.

Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Muliro Jumanne Muliro alisema ajali hiyo imehusisha gari lenye namba za usajili T 232 BQR TOYOTA NOAH iligongana uso kwa uso na semi teller lenye namba za usajili T198 CBQ/T283 CBG iliyokuwa ikitokea Tinde kuelekea Nzega.

Muliro alikitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa kwa taarifa za awali ni uzembe wa dereva wa Noah kuamua kuyapita magari yaliyokuwa mbele yake bila kuchukua tahadhari na hatimaye kugongana uso kwa uso na lori hilo.

Muliro alisema Noah hiyo ni mali ya Mwinyi Khamis wa Tinde na ilikuwa ikiendeshwa na Seif Mohamed (32) mkazi wa Tinde na lori hilo ni mali ya Aloyce Kavishe (46) mkazi wa Dar es salaam na ambaye pia alikuwa dereva wa gari hilo.

Kamanda Muliro alisema ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 18 kati yao wanaume 7 , wanawake 9 na watoto wawili wa kike wenye umri wa kati ya miaka 3- 5.

Kamanda Muliro aliwataja watu 10 waliotambuliwa kufariki kwenye ajali hiyo kuwa ni Daudi Maja, Dina Masanja, Chausiku Kasapa, Specioza Dotto, Ester Kasapa, Vicent Nzamala, Emmanuel Jumanne, Maganga Lubala, Debora Maingu na Andrea Mambosasa na tayari ndugu zao wanafanya maandalizi ya kwenda kuwafanyia mazishi.

Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga na imeanza kutambuliwa na ndugu zao.

Alisema madereva wote wa Noah Seif Mohamed na Aloyce Kavishe wa roli wote wanashikiliwa na Jeshi la polisi kwa mahojiano juu ya kukiuka sheria za usalama barabarani na kupoteza maisha ya abiria hao na majeruhi, na watafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga Dkt. Daniel Maguja alithibitisha kupokea miili ya marehemu 18 na majeruhi hao watatu ambao ni Hamis Ally (05) Salima Kiiza(01) na Boniface Richard na hali zao ni nzuri na wanaendelea kupatiwa tiba na waliumia sehemu mbalimbali za viungo vyao.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post