ASKARI POLISI WAFUKUZWA KAZI KWA KUDHALILISHA WANAFUNZI WA KIKE WAKATI WA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE 2016

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na shughuli zake za kila siku ili kuhakikisha mkoa unakuwa salama hii ni kutokana na wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili kuweza kuwabaini wahalifu wanaofanya vitendo vya uhalifu ili mkoa wetu uwe salama. 

Hata kuanzia tarehe 01.11.2016 Jeshi la Polisi lilianza zoezi la ulinzi wa Mitihani ya Kitaifa ya kuhitimu kidato cha nne 2016 katika Shule mbalimbali za mkoa wa mbeya. Hata hivyo katika zoezi hilo linaloendelea la ulinzi wa mitihani kuna changamoto zilijitokeza:-

KUFANYA KITENDO KIBAYA KINYUME NA MAADILI.
Mnamo tarehe 04.11.2016 majira ya saa 23:30 usiku huko katika Shule ya Sekondari Isuto iliyopo Kijiji na Kata ya Isuto, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi, Mkoa wa Mbeya, askari wawili wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya waliofahamika kwa majina ya 1. H.4925 PC PETRO OSCAR MAGANA wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya na 2. J.1422 PC LUKAS JOSEPH NG’WEINA wa Wilaya ya Kipolisi Mbalizi walituhumiwa kuwafanyia vitendo vibaya kinyume na maadili wanafunzi wa kike wa kidato cha nne wa Shule hiyo.

Inadaiwa kuwa, askari hao kwa pamoja wakiwa kwenye ulinzi wa mitihani ya kitaifa ya kidato cha nne 2016 waliwatoa kwenye Hostel wanafunzi wa kike kwa kile walichodai kupiga kelele.

Baada ya kuwatoa wanafunzi hao, waliwapeleka eneo la kufoleni na kuanza kuwapa adhabu mbalimbali ambazo ni kupiga push up, kuruka kichura, kushika masikio na kuwachapa viboko sehemu za makalio vitendo vilivyowasababishia maumivu makali na kupelekea baadhi ya wanafunzi hao wa kike kuondoa na kuelekea nyumbani kwao.

Kufuatia vitendo hivyo, Mkuu wa Shule hiyo aitwaye ROSE MZEE DIHEMBE alitoa taarifa kwa uongozi wa Wilaya ambapo taarifa zilifika kwa uongozi wa Mkoa ambao mara moja walifika eneo la tukio na kuchukua hatua za awali ikiwemo kusikiliza malalamikio hayo ya tukio na kuwaondoa askari waliolalamikiwa na mwisho kuchukua hatua za kinidhamu zilizopelekea kufukuzwa kazi askari hao.

Hata hivyo, kutokana na vitendo walivyovifanya askari hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara baada ya uchunguzi kukamilika.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito wananchi waendelee kuliamini Jeshi la Polisi kwamba halitafumbia macho vitendo vya askari vinavyokwenda kinyume na maadili ya kazi yao. Pia vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria za nchi. 

Aidha Kamanda KIDAVASHARI anaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa ya vitendo vyote vya uhalifu vinavyotendwa bila kujali vinatendwa na askari au wananchi wa kawaida ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Imesainiwa na:

[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]

KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post