Vurugu CCM na CHADEMA Shinyanga: DIWANI WA CHADEMA ANUSURIKA KUCHAPWA MAKONDE BAADA YA KUMKATIA WAYA DIWANI WA CCM


Ofisa wa Jeshi la Polisi akiendelea kutuliza jazba za madiwani wa Chadema

*****  
Kumetokea vurugu za aina yake katika baraza la madiwani wa manispaa ya Shinyanga baada ya madiwani hao kutoelewana na kutaka kuchapana makonde kavu kavu kwenye kikao chao cha baraza cha kawaida baada ya madiwani wa Chadema kuanzisha vurugu kwa madai ya kuonewa kwenye kikao hicho. 


Vurugu hizo zimeibuka leo baada ya madiwani wa Chadema wakati wakiomba muongozo wa kanuni kwenye kikao hicho huku mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni naibu meya wa manispaa hiyo Agnes Machiya akidaiwa kuwapuuza na kuruhusu kikao kuendelea ndipo hali ya hewa ilipochafuka. Wakati vurugu hizo zilizoenda sambamba na kupiga meza na kelele za hapa na pale zikiendelea, naibu Meya Agnes Machiya alimruhusu diwani wa kata ya Kambarage Hassan Mwendapole (CCM) kuendelea kusoma taarifa yake ya kata.

Wakati Mwendapole akiendelea kusoma taarifa yake diwani wa Chadema kata ya Ngokolo Emmanuel Ntobi aliinuka huku akimtolea lugha chafu diwani huyo kisha kukata waya wa kipaza sauti alichokuwa anatumia Mwendapole. Baada ya waya huo kukatwa huku meza zikiendelea kupigwa kwa fujo ndipo diwani Mwendapole alijawa na hasira na kutaka kumchapa vibao diwani wa Chadema Emmanuel Ntobi katika kikao hicho.

Kufuatia hali hiyo diwani wa viti maalumu Mariam Nyangaka (CCM) aliinuka na kumtuliza Mwendapole kisha kumtoa eneo la tukio. "Haiwezekani ufanye fujo halafu ukate na waya wewe ni mtoto mdogo nitakulamba makofi, usalama mnafanya nini humu toeni nje hawa sisi tuendelee na kikao wameshazoea kususa hata Dar es salaam ilikuwa hivyo CCM tukachukua umeya," alisikika akiongea Mwendapole.
Vurugu hizo ziliendelea mpaka pale ofisa wa jeshi la polisi aliyekuwepo kwenye kikao hicho kuingilia kati na kutuliza ghasia hizo. 


Madiwani wa Chadema mara kwa mara wamekuwa wakimtuhumu naibu meya Agnes Machiya kuendesha vikao kibabe kwa kutofuata miongozo na kanuni za vikao na kudaiwa kuwanyanyasa madiwani wa Chadema na kuwabeba madiwani wa CCM.

Baraza hilo la madiwani limejadili ajenda mbalimbali ambapo kitakaa ndani ya siku mbili kwa kusoma taarifa mbalimbali kwa mstakabali wa maendeleo ya wakazi wa mjini Shinyanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post