RAIS MAGUFULI AWALILIA WATU 10 WALIOFARIKI KWENYE AJALI YA BASI LINDI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bw. Godfrey Zambi kufuatia vifo vya watu 11 vilivyosababishwa na ajali ya basi la kampuni ya Barcelona iliyotokea jana tarehe 17 Oktoba, 2016 katika eneo la Miteja Wilaya ya Kilwa Mkoani Lindi.

Basi hilo lenye namba T 101 CUU lililokuwa likisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Kijiji cha Mahuta katika Wilaya ya Newala Mkoani Lindi, lilipinduka baada ya gurudumu lake la kushoto kupasuka na kusababisha vifo vya watu 10 papo hapo na mwingine 1 kufariki dunia baadaye akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Lindi, huku watu wengine 43 wakiwa wamejeruhiwa.

Katika salamu zake, Rais Magufuli amesema amepokea taarifa za vifo vya watu hao kwa mshituko na huzuni kwa kuwa kwa mara nyingine Taifa limepoteza watu wake na familia zimepoteza wapendwa wao na watu ambao ziliwapenda na kuwategemea.

"Ndugu Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bw. Godfrey Zambi naomba unifikishie salamu nyingi za pole kwa wote waliopoteza jamaa na ndugu zao katika ajali hii, kwa hakika nimeguswa sana na vifo hivi na naungana na familia za marehemu wote katika maombolezo na sala" amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli amewasihi wote walioguswa na vifo hivyo kuwa na moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi na amewaombea Marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina.

Pia Rais Magufuli amewaombea majeruhi wote wapone haraka ili waungane na familia zao na kurejea katika shughuli za ujenzi wa Taifa,
 
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Oktoba, 2016.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post