NAIBU MEYA APANDISHWA KIZIMBANI KWA KUTAPELI MILIONI 8 ZA MRADI






ALIYEKUWA Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Prosper Msofe (Chadema), na Ofisa Mtendaji wa kata ya Daraja Mbili jijini hapa, Modestus Lupogo wamesomewa maelezo ya awali katika kesi ya kujipatia Sh milioni nane kwa njia ya udanganyifu, fedha iliyokuwa imetolewa kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa maji.

Msofe, ambaye pia ni diwani wa kata ya Daraja Mbili na mwenzake walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Augustine Rwizile jana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru).

Akisoma maelezo hayo wakili wa Takukuru, Hamidu Simbano alidai mahakamani hapo kuwa Msofe akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya kata na Lupogo akiwa Katibu, Mei 13 mwaka 2013 wakiwa katika kikao walikubaliana kuomba kiasi cha Sh milioni 15 kutoka halmashauri ya jiji hilo kwa ajili ya mradi wa usambazaji wa maji katika mitaa ya Alinyanya na Sanare.

Simbano alidai kuwa Oktoba 4 mwaka 2013, halmashauri hiyo ilitoa Sh milioni nane kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na wakati mchakato huo ukiendelea Februari 13, Msofe aliandika barua kwa menejimenti ya kiwanda cha Sunflag kilichopo jijini hapa na kuomba ufadhili wa mradi huo wa maji.

Wakili Simbano alidai mahakamani hapo Machi 5, menejimenti hiyo ilikubali kufadhili mradi huo na Juni kiwanda hicho kilikubali kutoa maji kwenye kiwanda chake na kugharamia gharama za kuyasambaza katika mtaa wa Alinyanya, hivyo kazi iliyokuwa imebaki ilikuwa ni kusambaza maji kutoka Alinyanya kwenda mtaa wa Sanare.

Alidai kuwa Msofe aliandaa taarifa ya mapato na matumizi ya Oktoba hadi Desemba mwaka 2013, iliyokuwa ikidai kuwa Sh milioni nane zimetumika kusambaza maji kutoka kiwanda cha Sunflag hadi mitaa ya Alinyanya na Sanare, jambo ambalo si kweli.

Wakili Simbano alidai mahakamani hapo kuwa upande wa Serikali utakuwa na vielelezo 20 na mashahidi 10 katika kesi hiyo.

Watuhumiwa wanakabiliwa na mashitaka matatu wanayodaiwa kuyafanya kati ya Oktoba Mosi na Novemba 2013. Kesi imeahirishwa hadi Novemba 16 mwaka huu itakapotajwa na kupangiwa tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Imeandikwa na Veronica Mheta-Habarileo Arusha

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post