MATOKEO YA MCHEZO WA WATANI WA JADI SIMBA NA YANGA OKTOBA 1,2016,KICHUYA ATULIZA PRESHA YA SIMBA

Jumamosi ya Oktoba 1 2016 ni siku ambayo mashabiki wa soka Tanzania wamepata nafasi ya kuangalia mchezo wa watani wa jadi kati ya Yanga na Simba uliofanyika katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam, ambao ulikuwa ni mchezo wa kwanza wa round ya Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2016/2017.

Dakika 90 za mchezo zimemalizika kwa timu ya Yanga na Simba kutoka droo kwa kufungana bao 1-1

Shiza Ramadhani Kichuya ameifungia Simba bao la kusawazisha katika mechi ya watani wa jadi iliyomalizika kwa sare ya kufungana goli 1-1.

Yanga walitangulia kupata bao kupitia Amis Tambwe lililofungwa dakika ya 27 kipindi cha kwanza.


 Goli hilo lilizua tafrani kwa wachezaji wa Simba kumzonga mwamuzi wa mchezo huo Martin Saanya hali iliyopelekea kumuonesha kadi nyekundu nahodha wa Simba Jonas Mkude.

Mashabiki wa Simba walianzisha vurugu kwa kung’oa viti na kuvirusha uwanjani hali iliyopelekea polisi kutumia mabomu ya machozi kuleta utulivu ndani ya uwanja.

Kipindi cha kwanza kikamalizika Yanga wakiwa mbele kwa goli 1-0 huku Simba wakiwa pungufu kufuatia Mkude kuoneshwa kadi nyekundu.

Zikiwa zimesalia dakika tatu mchezo kumalizika, Simba walipata kona ambayo ilipigwa na Kichuya na kutinga moja kwa moja wavuni.


Kwa muda mrefu ukizungumza habari ya soka la Tanzania, lazima uguse uwepo wa vilabu viwili vya Simba na Yanga ambavyo vimetokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo ushirikiano wa vijana katika shughuli mbalimbali pia ikichangia kuanzishwa kwa timu hizi.


Yanga ndiyo kongwe kiumri ikiwa imeanzishwa rasmi mwaka 1935 Simba ikifuata mwaka mmoja baadaye 1936 ikiitwa Sunderland jina ambalo lilitokana na timu mojawapo ya ligi ya England wakati Yanga ilikuwa ikifahamika kwa jina la Young Africans SC ambalo ni chimbuko la jina la kimarekani.
Baadaye viongozi wa serikali walivitaka vilabu hivi kubadilisha majina yao na kutumia majina halisi ya kiafrika na kuondoka kwenye majina ya kigeni, hapo ndipo tukapata Simba na Yanga.



Vilabu hivi vimejenga upinzani mkubwa katika soka la Tanzania tangu mwaka 1936 wakati huo ikichezwa ligi ya mkoa wa Dar es Salaam (Dar es Salaam League) hadi mwaka 1965 ilipoundwa ligi ya taifa lakini hadi leo vimekuwa vikiumiza vichwa vya mashabiki lukuki wa soka ndani na nje ya nchi kutaka kujua nani ataibuka na ushindi pale vidume hivi viwili vinapokutana.


Matokeo yoyote ya timu hizi hugusa mashabiki kwa hisia tofauti, wengine huwa na shangwe kubwa wakati upande mwingine wakilia na kupoteza fahamu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527