MAHAKAMA ZAWEKA MUDA MAALUM KUSIKILIZA KESI ZA MAFATAKI,KUSIKILIZWA KWENYE KATA

WILAYA ya Tunduru mkoani Ruvuma imetenga muda maalumu mahakamani kusikiliza kesi na mashauri yanayohusu wanaume wanaowapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Homera wakati akizungumza na wanafunzi na wazazi wa Shule ya Sekondari Wasichana ya Masonya katika mahafali ya 11 ya kidato cha nne kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Homera alieleza kuwa imebainika kuwa kushuka kwa ufaulu kwa wasichana wengi katika shule za sekondari wilayani humo, kunachangiwa na wanafunzi wa kike kujihusisha na mapenzi na hivyo kuwafanya kutozingatia masomo.

Alisema ili kukomesha hilo, ameiagiza Idara ya Mahakama kuendesha kesi za watu wanaotuhumiwa kuwapa mimba wanafunzi zifanyike kwenye kata ili kuharakisha usikilizaji wa kesi kwa kuwarahisishia mashahidi kutokwenda mbali pamoja na kesi kuchukua muda mrefu na nyingine hufikia mwisho wakati muda wa kuhitimu masomo ulishapita.

Aidha, mkuu huyo wa wilaya, aliwapongeza walimu wa shule hiyo kwa kutoa elimu kwa kiwango cha juu na kuifanya shule hiyo kuongoza kimkoa na kuwa miongoni mwa shule bora 100 kitaifa katika mitihani ya kidato cha sita mwaka jana na kuwataka wanafunzi wa kidato cha nne kuweka rekodi ya kuondoa daraja la nne.

Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa shule hiyo, Elice Banda amewataka wazazi kuwapatia watoto wao mahitaji yote muhimu ili kuepuka kushawishika kupokea misaada kwa 'mafataki'.

Alisema shule hiyo ina wanafunzi wa kike 533 wa kidato cha kwanza hadi cha sita, na inakabiliwa na uhaba wa malazi kutokana na mabweni kutokidhi wingi wao.

Imeandikwa na Muhidin Amri - Habarileo Tunduru

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post