BAADA YA CCM KUMSHAMBULIA LOWASSA..CHADEMA YASISITIZA KUWA LOWASSA NA UKAWA NI TISHIO CCM


Baada ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia msemaji wake Christopher Ole Sendeka kusema kuwa aliyekuwa mgombea wa kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Edward Lowassa, kuwa si tishio kwa CCM.

Jumamosi ya Oktoba, 29 Chadema imejibu kuwa Lowassa pamoja na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) utaendelea kuwa tishio kwa chama hicho na kwamba CCM ijiandae kuachia madaraka mwaka 2020 kwa kuwa imejipanga kuchukua dola.

Mkuu wa Idara ya Uenezi Chadema Taifa, Hemed Ali wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam amesema Lowassa ni tishio kwa kuwa alipokihama chama hicho aliacha mpasuko na kudai kuwa aliondoka na nguvu ya chama hicho.

“CCM wana homa kubwa iitwayo Lowassaphobia na ndio maana imeacha kuendelea na shughuli zao na kumuandama Mjumbe wa kamati kuu wa chama chetu Lowassa. Kimsingi mchakato wa kumpata Mgombea Urais na Mgombea mwenza wa chama chetu ulikuwa wa kidemokrasia kwa mujibu wa katiba yetu ambapo ibara (7.7.16 (a) kamati kuu inapewa mamlaka ya kuwafanyia utafiti wagombea Urais wa chama chetu na kupeleka ripoti Baraza kuu,

“Baraza kuu la chama kwa mujibu wa katiba ( 7.7. 13 (a)) inapendekeza majina ya wagombea au mgombea aliejitokeza na hatimae kwa mujibu wa katiba (7.7.10 (c)) Mkutano mkuu wa chama utachagua mgombea Urais na Mgombea Mwenza,” amesema na kuongeza.

” Lowassa alipitia hatua zote kama mwanachama halali wa CHADEMA mwenye haki sawa na mwanachama yeyote kwa mujibu wa katiba (5.1) na (5.2) kimatendo na kiimani kwa kufuata katiba , nilitaraji Sendeka aeleze kile kiini macho cha kumchagua Ndugu Magufuli Dodoma kuwa Mgombea wao huku wenyewe kwa wenyewe wakipinga mchakato wa kumpata usiofuata katiba na kanuni za chama hicho kama walivyojitenga na uamuzi huo baadhi ya wajumbe wa kamati kuu ile kutokana na kutoridhishwa na mwenendo wa maamuzi ndani ya vikao.”

Amedai kuwa, Kamati Kuu yao ilipasuka katikati baina ya wajumbe wake na kudai kuwa wajumbe waliokuwa wanamuunga mkono Lowassa, wengi wao hawakuchaguliwa kushika nyadhifa serikalini .

“Ni kawaida ya CCM kuchafua mtu ambae atakua na msimamo na nia ya kulivusha taifa , Wamefanya hivyo kwa viongozi wetu wa chama na watu binafsi hivyo hatushangai walivyo mshambulia Lowassa akiwa ndani ya CCM na hata Sasa CHADEMA. Sendeka amesema kuwa yupo kiongozi ndani ya chama chetu aliyepata dola milioni 15 takribani bilioni 33 eti apangesafu ya uongozi ndani ya chama,

“Kiuhalisia na kwa hesabu ndogo tu ni kuwa pesa hiyo si tuu kuwa inatosha kwa ajili ya kupanga uongozi ndani ya chama bali ni inatosha kwa ushindi wa mitaa, kata na halmashauri , ubunge na urais hivyo wakati anataja tarakimu hizo ajue na michanganuo ya kimahesabu badala ya kuwa mkurupukaji na ningemuelewa kama angekuja hadharani kuaga rasmi kwa niaba ya chama chake na kutupisha kuwatumikia watanzania kuliko kuongea uongo,” amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post