RAIS MAGUFULI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI AJALI ILIYOUA WATU 13 MWANZA

Rais Dkt. John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella kufuatia vifo vya watu 13 vilivyosababishwa na ajali ya barabarani iliyotokana na basi la abiria la Kampuni ya Super Shem kuligonga basi dogo la abiria (Daladala) katika kijiji cha Mwamaya kilichopo katika Kata ya Hungumalwa, Wilaya ya Kwimba Mkoani Mwanza.

Ajali hiyo imetokea leo saa 12:15 asubuhi baada ya basi hilo dogo lililokuwa likitoka Kijiji cha Shirima kwenda Nyegezi Mjini Mwanza kuingia ghafla barabara kuu na kisha kugongwa na basi la Kampuni ya Super Shem lililokuwa likitoka Mkoani Mbeya kwenda Mwanza.

Katika ajali hiyo watu wote 13 waliopoteza maisha na majeruhi 15 waliolazwa hospitali walikuwa abiria wa basi dogo lililogongwa.


Rais Magufuli ameelezea kupokea taarifa za ajali hiyo kwa mshituko mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa imetokea siku moja tu tangu Watanzania wengine 12 wapoteze maisha katika ajali ya basi la Kampuni ya New Force iliyotokea katika kijiji cha Lilombwi, Kata ya Kifanya, Tarafa ya Igominyi Mkoani Njombe.

"Nimesikitishwa sana na vifo vingine vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha katika ajali huko Mwanza, nakuomba Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella unifikishie salamu za pole kwa familia zote zilizopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali hii.

 "Nawaombea wote waliotangulia mbele za haki wapumzishwe mahali pema na pia wote walioguswa na msiba wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi kigumu cha majonzi ya kuondokewa na jamaa zao," amesisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amewaombea majeruhi wote wa ajali hii wapone haraka ili waungane na familia zao na kuendelea na shughuli za ujenzi wa Taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post