PROFESA LIPUMBA AENDELEA KUUNG'ANG'ANIA UENYEKITI CUF LICHA YA KUNG'OLEWA UANACHAMA

MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa bado anatambua yeye ni mwenyekiti halali wa chama hicho, kwa kuwa wenye mamlaka ya kumvua madaraka ni Mkutano Mkuu ambao huwashirikisha wajumbe kutoka Bara na Zanzibar.


Aidha amesema atampokea Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad siku atakapofika kwenye ofisi hiyo makao makuu Buguruni kwa ajili ya kuandaa mikakati ya kukijenga chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Profesa Lipumba alisema kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kilichofanyika Zanzibar ni batili kwa kuwa walikiuka katiba ya chama hicho.

Profesa Lipumba alisema, kwa mujibu wa kifungu cha 79(2)(a) cha katiba ya chama hicho kinasema kuwa, Mkutano Mkuu wa Taifa unaweza kuchukua hatua za kinidhamu zozote zile, zikiwamo kumuachisha au kumkufukuza uongozi au uanachama au yote mawili Mwenyekiti wa chama hicho.

Alisema kutokana na kifungu hicho, “Mimi navuliwa uanachama na Mkutano Mkuu wa Taifa, sio baraza la uongozi ambalo na lenyewe halijakidhi matakwa ya katiba ya chama, kilichofanyika Zanzibar ni sawa na kikao cha harusi,” alisema.

Alisema pamoja na kufanyika kwa kikao hicho, lakini pia idadi ya wajumbe waliohudhuria kutoka Bara ni 9 ambao kati yao, watatu wajumbe wa kamati kuu na sita ni wanachama wa kawaida, wakati Katiba ya chama hicho kinawataka kuwa na wajumbe 22 kutoka Kamati Kuu ya chama.

Profesa Lipumba alisema, katika katiba hiyo, pia kifungu cha 83(5) kinasema, baraza hilo linaweza kuchukua hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kutoa onyo kwa maandishi, karipio kali.

Alisema, kabla ya kufikia uamuzi huo, Katibu Mkuu alipaswa kuitisha Mkutano Mkuu ambao pamoja na mambo mengine, ulitakiwa kumjadili ili wajumbe waweze kumpigia kura ya kumwondoa. Pia alisema alipaswa kupewa nafasi ya kujieleza katika mkutano mkuu ndipo wajumbe waamue hatua ya kumchukulia.

Kutokana na hayo alisema yeye bado ni mwenyekiti halali na yupo ngangari katika kukijenga chama na hafukuziki, hasusi wala hawezi kukihama chama hicho badala yake amejiwekee mikakati ya kuhakikisha anawaunganisha wanachama wa chama hicho.

Hata hivyo alisema katika kipindi hiki ambacho chama hicho kimetoka kwenye mgogoro wa uongozi uliosababisha Msajili wa vyama vya siasa kuingilia kati, wanapaswa kukaa pamoja na kuondoa tofauti zilizopo ili waweze kukijenga chama.

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema jana kuwa, haijapokea mabadiliko yoyote ya uongozi kutoka katika chama hicho, hivyo wanaendelea kumtambua Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho.

Aidha, ofisi hiyo ya msajili wa vyama vya siasa imesema msimamo wake upo pale pale kwamba Lipumba ni Mwenyekiti halali wa CUF kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho mpaka hapo itakapoelezwa tofauti kwa kusimamia sheria za vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho.

Hivi karibuni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa msimamo wa msajili ni kwamba bado Lipumba ni Mwenyekiti halali wa CUF na wanachama wote waliofukuzwa uanachama na kikao cha Baraza Kuu la Uongozi cha Agosti 28 mwaka huu ni halali.

Alitoa angalizo kuwa, kamati iliyoundwa kuongoza chama na viongozi walioteuliwa si halali na kwa kuwa kifungu cha 8B (2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye si kiongozi wa chama haruhusiwi kufanya kazi za chama kama viongozi, ofisi yake haiwatambui viongozi hao.
Chanzo-Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527