Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DIWANI WA CHADEMA KUTUA KWA RAIS MAGUFULI KUFIKISHA KERO YA MAJI SHINYANGA

Diwani wa kata ya Ngokolo katika manispaa ya Shinyanga Emmanuel Ntobi kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) amedhamiria kwenda kuishitaki Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Shuwasa mjini Shinyanga kwa rais John Magufuli kwa kupandisha bei za maji kinyemela kwa wakazi wa mji wa Shinyanga hali ambayo imekuwa kero kubwa kwao.


Akizungumza na vyombo vya habari juzi diwani huyo alisema, ikiwa yeye ni mwakilishi wa wananchi hivyo hana budi kupaza sauti za wanyonge katika kuwatetea pale wanapoonewa kwa kupandishiwa bei za maji kinyemela, na hivyo kuwafanya baadhi yao kushindwa kulipa na kurudi kutumia maji machafu ambayo ni hatari kwa afya zao.


Ntobi alisema katika kikao walichokaa na Ewura mwaka jana wakishirikiana na wananchi juu ya kujadili kupandishwa kwa bei ya maji mjini humo hawakukubaliana nayo kutokana na wakazi wa eneo hilo kuwa na vipato vya chini, lakini cha ajabu mamlaka hiyo ya maji Shuwasa imepandisha bei kinyemela.


“Kisheria ninavyo fahamu ili bei ya maji ipandishwe lazima Mamlaka ya maji ishirikiane na EWURA wakiwamo na wananchi wenyewe kama wataridhia bei hiyo ipandishwe, lakini katika kikao hicho tulikataa, hivyo ilipaswa bei ya zamani ya uniti (1) 7,900 ibaki na siyo kuletewa bei ya 1,105 huu ni uonevu,”,alisema Ntobi.



“Nimeandika barua kwenda kwa Ewura, ni muda mrefu sasa haijibiwi hivyo nao inawezekana wanabariki uonevu huu,na nimetoa muda wa mwisho wasipojibu malalamiko yetu mimi kama diwani nitakwenda kwa rais kushitaki ili hatua za kisheria zichukuliwe watu wapate maji safi kwa gharama nafuu”,aliongeza Ntobi. 


Aidha diwani huyo aliongeza kuwa hata usomaji wa mita za maji wa mamlaka hiyo haufanyiki kwa ufasaha na wahusika wanadaiwa kutofika kwenye makazi ya watu, bali wanaleta bili kwa maksio kwa kupitia ujumbe mfupi wa simu, na hivyo kuzidisha bili mara mbili yake na kusababisha kuwaibia wananchi. 


Kwa upande wake mkurugenzi wa mamlaka hiyo ya maji (SHUWASA), Injinia Silvester Mahole akijibu malalamiko hayo alisema, wameamua kupandisha bei hiyo ya maji kutokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji na matengezo, huku akikiri hapo awali kulikuwa na watumishi ambao walikuwa wakileta takwimu za mita siyo sahihi.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com