RAIS SHEIN KESHO KUZINDUA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR


Rais wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ) Dk Ali Mohamed Shein kesho atazindua Baraza la Wawakilishi la tisa huku akitarajia kutoa mwelekeo wa Serikali yake mpya iliyopatikana baada ya Uchaguzi wa Marudio wa Machi 20 uliotawaliwa na mgawanyiko wa kisiasa.


Tofauti na hotuba yake ya ufunguzi ya Novemba 2010, Dk Shein atahutubia baraza hilo likiwa na wabunge wa chama kimoja cha CCM baada ya vyama vya upinzani vilivyotangaza kushiriki uchaguzi wa marudio kushindwa kupata viti vya uwakilishi.


Pia, atahutubia akiwa bado hajamteua Makamu wa Kwanza wa Rais kutokana na matokeo ya uchaguzi huo kutofanikisha kupatikana chama cha upinzani chenye kura zisizopungua asilimia 10 za kufanikisha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).


Chama kikuu cha upinzani cha CUF na vingine tisa vilisusia kushiriki uchaguzi huo baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 kufutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutokana na sababu za uvunjifu wa taratibu na sheria za uchaguzi.


Hata hivyo, majina ya wagombea wa vyama hivyo yalijumuishwa kwenye karatasi za kura na kusababisha kuvuna kura kidogo ambazo hazikitosha kutoa Makamu wa Kwanza wa Rais na Wawakilishi ambao miongoni mwao huteuliwa kuwa mawaziri wa SMZ.


Tayari Dk Shein alishaeleza kiufupi baada ya kuapishwa majuma mawili yaliyopita kuwa Serikali yake itakuwa shirikishi kwa kujumuisha upinzani na haitabagua katika utoaji wa huduma za jamii katika kuwaletea wananchi maendeleo.


Jambo kubwa ambalo Wazanzibari wengi wanasubiri kulisikia kutoka kwa kiongozi huyo ni iwapo ataeleza kinagaubaga namna atakavyokabiliana na mtanzuko wa kikatiba wakati wa uundaji wa SUK.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post