Madiwani wa Chadema Manispaa ya Shinyanga Watoa Tamko Kupinga Mradi wa Kuelimisha Watu Wanaofanya Biashara ya Kuuza Miili Yao


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.

TAMKO LA MADIWANI WA CHADEMA HALMASHAURI YA MANISPAA SHINYANGA KUPINGA AZIMIO LA KURUHUSU SHIRIKA LISILO LA KISERIKALI LA RAFIKI SDO KUFANYA SHUGHULI ZAKE KWA "MASHOGA" NA "MACHANGUDOA" KATIKA MANISPAA YA SHINYANGA.


Mapema wiki iliyopita, wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na Watanzania kwa ujumla, wamepatwa na sintofahamu kubwa, baada ya kusikia na kusoma kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii, kuwa baraza la madiwani Manispaa ya Shinyanga limetoa ruksa kwa shirika lisilo la kiserikali la Rafiki SDO kufanya“mradi tata”wa Makaka Poa “Mashoga” na Madada poa “Machangudoa” katika Manispaa ya Shinyanga. 


Katika kikao cha baraza la madiwani Manispaa ya Shinyanga kilichofanyika Alhamis ya tarehe 7/4/2016. Kikao hicho kilichoitwa cha “dharula”kilikuwa na ajenda moja tu ya kuruhusu ama la, shughuli za shirika hilo kufanya kazi katika Manispaa. Hoja hiyo ilipitishwa kwa kuungwa mkono na madiwani / wajumbe kutoka CCM. Katika kikao hicho Madiwani wa CHADEMA tulipinga kupitishwa kwa azimio hilo. Ifahamike kuwa,Shinyanga ina jumla ya madiwani 23,CHADEMA 07, CCM 16.


Mosi,Madiwani wa CHADEMA katika Halmashauri ya Shinyanga, tulipinga ndani ya kikao na tunaendelea kupinga kwa nguvu zetu zote, azimio hilo la kuruhusu Shirika la Rafiki SDO, ambalo linataka kufanya mradi wake pamoja na mambo mengine ni kutoa elimu ya kutumia vilainishi (mafuta maalumu ya kutumia wakati wa kujamiina) kwa wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao "Mashoga" na kwa wanawake wanauza miili yao “Machangudoa ", kwa kigezo cha kupunguza maambukizi ya UKIMWI. 

Kwamba, tunapinga mradi huu kwa sababuhauendani kabisa na maadili, mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania na Mwafrika . hivyo mradi huu ni hatari kwa kuharibu maadili na utamaduni wetu kuwahi kutokea Tanzania na Afrika kwa ujumla. .

. Kwamba, tunapinga mradi huu kwa sababu unapingana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, na sheria za nchi yetu, hakuna mahali ambapo kumetambuliwa uwepo wa watu wanaitwa "Mashoga" na "Changudoa" kama ni makundi katika jamii yetu ambayo shirika hili linataka kufanya nao kazi ya kuwasaidia. .

Kwamba, tunapinga azimio hilo kwa sababu tunahisi kuna hali ya rushwa kwa baadhi ya madiwani wa CCM katika kufikia azimio hili la kuruhusu mradi wa shirika la Rafiki SDO, huku wakitambua mradi huo unakiuka Katiba, sharia za Nchi, maadili na utamaduni wa Mtanzania, na kuchukua tamaduni za kimagharibi. Kama wawakilishi walipaswa kupinga mradi huu kama hapo awali tulivyopinga pande zote. 


Hivyo tunasema, hakuna uhusiano wa kilichoandikwa katika muhtasari wa shughuli za shirika hilo na uhalisia uliopo mtaani, kuwa shirika hilo limedai linatoa elimu ya ujasiriamali kwa “Mashoga” na “Machangudoa” . Tunahoji kama wanatoa elimu ya ujasiriamali, Ni kwa nini iwe kwa mashoga na machangudoa tu? Ilhali yapo makundi mengine kama ya akina mama, vijana, watu wenye ulemavu na wengine walio katika mazingira magumu. 
Lakini pia, ni njia zipi ambazo wametumia kuwatambua walengwa wa huo mradi hasa mashoga?Kwa nini wanaibagua jamii yetu kwa matendo ya hovyo? Maswali haya ndiyo yanatupa majibu kuwa kuna ulakini katika shughuli za shirika hili.

Mwisho, Tunaitaka Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ifanye haraka sana yafuatayo.

Mosi , tunamtaka waziri mwenye dhamana ( kwa maana ya serikali kuu) kuingilia kati na kusimamisha mara moja shughuli za shirika la Rafiki SDO, lisiendelee na kazi zake katika manispaa ya Shinyanga. kwa sababu mradi huu umekwishakuwa na utata kwa jamii.

Kwamba, tunataka kufanyike uchunguzi wa kina, kujiridhisha juu ya malengo na maudhui ya shirika hili la Rafiki SDO na mradi wao kwa jamii ya Tanzania. 


Kwamba, tuitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambanana Rushwa TAKUKURU, kufanya uchunguzi wa kina kwa baadhi ya madiwani wa CCM ili kubaini, wapi wametoa msukumo wa kuvunja katiba, sheria za nchi, Maadili na Utamaduni wa Mtanzania na kukiuka kiapo chao. 


Madiwani CHADEMA kamwe hatutokubali kuona kizazi hiki cha kitanzania kinanaharibiwa kwa sababu ya faida ya watu wachache na familia zao. 


Mwisho kabisa tunawaomba viongozi wa dini mbalimbali,wanashinyanga na watanzania wote kwa ujumla,wakiwemo, wandishi, kutuungamkono kupinga kwa nguvu zote vitendo hivi ambavyo ni dhahiri vikiachwa vitaharibu maadili na utamaduni wetu watanzania.

Mabadiliko Daima.

Asanteni,

Imetolewa leo, Ijumaa Aprili 15, 2016 na :

Emmanuel Ntobi
Mwenyekiti wa madiwani CHADEMAMANISPAA YA SHINYANGA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post