JARIBIO LA KUMWONDOA MARADAKANI RAIS ZUMA LASHINDIKANA


Jaribio la kutaka kumuondoa madarakani Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma limegonga mwamba baada ya idadi ya kura zilizohitajika bungeni kushindwa kutimia.


Wabunge walitaka kumng’oa Rais Zuma kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Rufani uliotolewa Alhamisi wiki iliyopita kuwa kiongozi huyo alikiuka sheria kwa kutumia mabilioni ya fedha za umma kukarabati makazi yake binafsi.


Upigaji kura ndani ya Bunge ulihitaji theluthi mbili ya wajumbe ili kumng’oa kiongozi huyo. Chama tawala cha African National Congress (ANC) kina idadi kubwa ya wabunge.


Katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufani iliamua kwamba Rais Zuma alikiuka katiba kwa kushindwa kurejesha sehemu ya Sh2.4 bilioni za umma alizotumia kukarabati makazi hayo yaliyopo eneo la Nkandla katika Mkoa wa Kwa Zulu-Natal.


Rais Zuma alitumia fedha hizo kujenga bwawa la kuogelea, mabanda ya kuku na ng’ombe na chumba maalumu cha burudani.


Ripoti iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Thuli Madonsela mwaka 2014 ilifichua kuwa familia ya kiongozi huyo ilitumia fedha hizo kinyume cha sheria. Thuli alimtaka rais kurejesha sehemu ya fedha hizo.


Ijumaa iliyopita, Rais Zuma aliomba msamaha kupitia luninga ya serikali, huku akisema amesikitishwa na kusononeshwa na sakata hilo. Zuma alisema atarejesha sehemu ya fedha anazodaiwa kuzitumia kama ilivyoagizwa na mahakama.


Hoja ya kutaka kumng’oa Rais Zuma iliwasilishwa bungeni na chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA). Viongozi wa upinzani walidai kuwa uongozi wake unafanya kinyume na ule wa Mwasisi wa Taifa hilo, Nelson Mandela.


“Jacob Zuma ni maradhi ya kansa ndani ya mioyo ya raia wa Afrika Kusini. Hafai kamwe kuongoza taifa,” ulisema upinzani uliokuwa ukijibu hotuba ya rais ya Ijumaa.


Baada ya Mahakama ya Rufani kutoa uamuzi wake , Kiongozi wa Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema alisema upinzani hautamruhusu Rais Zuma kulihutubia tena bunge.


“Kuanzia leo hatutamruhusu rais kuhutubia Bunge kwani tutamnyamazisha kwa nguvu. Tutamfurusha bungeni kwa kuwa kuanzia sasa yeye siyo Rais wa Afrika Kusini,” alisema Malema.


Vigogo wa ANC waliomsaidia Hayati Mandela kuingia madarakani mwaka wa 1994, wamemtaka Rais Zuma kujiuzulu ili kukiondolea fedheha chama hicho.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post