BUNGE LAANZISHA STUDIO KWA AJILI YA KURUSHA MATANGAZO YA BUNGE LA TANZANIA

 
Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye amesema uamuzi wa serikali kuzuia matangazo TBC kutokurusha moja kwa moja(live) matangazo ya Bunge ilikuwa na lengo la kulinusuru shirika hilo lisife kwani lilikuwa likitumia fedha nyingi kwa ajili ya matangazo hayo .


Amesema uamuzi huo ni mkakati wa kuliwezesha shirika hilo kuweza kujiendesha kwani awali lilikuwa likitumia fedha nyingi kwa urushaji wa matangazo ya bunge bila ya malipo.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, amesema hayo jijini Mbeya, wakati akizungumza na wadau wa habari, michezo, utamaduni na watendaji wa serikali mikoa ya Mbeya na Songwe,


Amesema shirika la utangazaji la Taifa, TBC, lilikuwa linaagizwa kurusha matangazo ya Bunge bila ya malipo ambapo kwa mwaka shirika lilikuwa likitumia bilioni 4 kwa mapato yake ya ndani na kulifanya kushindwa kukarabati mitambo pamoja na mslahi ya watumishi hivyo, uamuzi huo ulikuwa sahihi licha ya wananchi wengi kuonesha kutoridhishwa no.


Amesisitiza kuwa suala hilo litaleta heshima ya Bunge kwani ilifika wakati, baadhi ya wabunge walikuwa wakitoa lugha za maudhi pamoja na kucheza sarakasi mambo ambayo yalikuwa yakivunja heshima ya bunge.


Amesema kutokana na hatua hiyo Bunge lenyewe ndio limechukua dhamana ya kuanzisha studio yake hivyo kutoa fursa kwa televisheni nyingine kurusha matangazo ya moja kwa moja lakini kulingana na vigezo na masharti yatakayohalalishwa na mamlaka hiyo.


Akizungumzia sheria ya baraza la michezo ambayo imekuwa ikilitaja suala la michezo ni hiari, Nape amesema kwa sasa serikali ipo katika mchakato wa kuirasimisha sheria hiyo ili iendane na sera ya michezo ambayo imeweka wazi kwamba michezo kuwa shughuli rasmi ya kiuchumi, ambapo katika kikao hicho wajumbe walipata nafasi ya kuwasilisha kero na changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo.


Aidha, akijibu risala iliyotolewa na Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Mbeya, ambayo ilimuomba kiongozi huyo kuhakikisha anausimamia mswada huo wa habari katika kulinda maslahi ya wafanyakazi,Nape, aliwataka waandishi wa habari kutambua kuwa maslahi yao wanayoyapigania kutoka kwa waajiri wao, yanajibiwa kwenye mswaada wa sheria ya huduma wa vyombo vya habari.


Alisema, wakati ule ulikuwa ni mwishoni mwa Bunge lililopita hivyo kwa sheria na kanuni za Bunge mswaada huo unatakiwa ukasomwe tena kwa mara ya kwanza, kwa hiyo umefikia pahala pazuri, na kuhakikisha kwamba maslahi ya waandishi wa habari mule ndani yamelindwa.


Pia, Waziri huyo, aliongeza kuwa serikali inaangalia utaratibu wa kuvifuta baadhi ya vyuo vinavyotoa elimu ya habari ambavyo havina sifa, kwani vimekuwa vikitoa waandishi wa habari amaboa hawana sifa na kazi yao imekuwa ni kuupotosha umma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527