Atupwa Jela Miaka 7 Kwa Kujeruhi Watu Wawili Kwa Kutumia WembeMahakama ya Wilaya ya Ilala, imemhukumu kifungo cha miaka saba jela fundi umeme, Lipyana Ndumbaro (29) baada ya kupatikana na hatia ya kujeruhi kwa kutumia wembe.

Mahakama pia imemtaka Ndumbaro kumlipa fidia ya Sh2 milioni mlalamikaji.

Ndumbaro ambaye ni mkazi wa Mvuti wilayani Ilala, hakuwapo mahakamani hapo wakati hukumu hiyo inatolewa baada ya kuruka dhamana.

Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi, John Msafiri alisema Mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi saba uliotolewa mahakamani hapo.

Hakimu Msafiri alisema Mahakama ilipokea vielelezo vitatu ambavyo ni picha, maelezo ya mgonjwa na fomu namba tatu ya Polisi (PF3).

“Kupitia ushahidi huu, Mahakama imeridhika na ushahidi wa upande wa mashtaka uliotolewa mahakamani hapa bila kuacha shaka,” alisema Hakimu Msafiri.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu, Wakili wa Serikali, Neema Moshi aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali ili liwe fundisho kwa watu wengine wanaofanya vitendo kama hivyo.

Katika hati ya mashtaka, ilidaiwa mshtakiwa alitenda matukio hayo kwa watu wawili tofauti.

Ilidaiwa Machi 17, 2014 maeneo ya Mvuti wilayani Ilala, alimkata kwa wembe Watunde Abdallah sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia maumivu.

Pia, tarehe na mwaka huohuo, alimkata kwa wembe Shaban Kivanga na kumsababishia maumivu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post