Aliyejilipa Mishahara Hewa 17 Afukuzwa TRA

 
Mfayakazi wa Mamlaka ya Mapato Nchini aliyetuhumiwa na Rais John Magufuli mwezi uliopita kujilipa mishahara 17 ya watumishi hewa, hayupo kwenye ajira ya TRA kwa siku nyingi zilizopita, imefahamika.

 
Habari kutoka ndani ya Mamlaka hiyo zimesema kuwa mfanyakazi huyo alikuwa ni wa Idara ya Uhasibu ya TRA lakini alishafukuzwa kazi siku nyingi zilizopita.

Chanzo cha kuaminika kutoka Makao Makuu ya TRA kimeiambia Nipashe kuwa mfanyakazi huyo alifukuzwa kazi baada ya kubainika kujilipa mishahara hiyo katika akaunti yake.

Chanzo chetu cha habari ambacho hakikupenda kutajwa jina gazetini kwa sababu si msemaji wa mamlaka, kilisema mfanyakazi huyo baada ya kuhojiwa alikiri kujilipa mishahara hiyo.

Ndipo alipochukuliwa hatua za kufukuzwa kazi pamoja na kufikishwa Mahakamani, kilisema chanzo hicho.

“Huyu mfanyakazi alikuwa Idara ya Uhasibu... ni kweli alijilipa mishahara hiyo na baada ya kuhojiwa alikiri ndipo tukamfukuza kazi na kumpeleka mahakamani,” chanzo hicho kilieleza.

“(Lakini) huyu si mfanyakazi wa TRA tena maana alivyohojiwa na kuthibitika kuwa ni kweli tulishamfukuza kazi.”

Rais Magufuli alimfichua mfanyakazi huyo hivi karibuni akiwa nyumbani kwake katika Kijiji cha Mlimani, Wilaya ya Chato mkoani Geita, alipokuwa alihutubia kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe kuwa Rais Oktoba 25, mwaka jana.

“Yupo mfanyakazi mmoja wa TRA ambaye alikuwa akijilipa mishahara ya watu 17 na huyo ni lazima afikishwe mahakamani,” alisema Rais Magufuli akionekana mwenye kuchukizwa na jambo hilo.

Pia hivi karibuni Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Imani Abduli Nyamangaro (44) alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida akikabiliwa na tuhuma za kujilipa mishahara hewa ya wastaafu 57 yenye jumla ya Sh. 29.4.

Mwendesha Mashtaka, Wakili wa serikali, Michael Lucas Ng’hoboko alidai kwamba kati ya Aprili 29, mwaka 2013 na Machi 27, mwaka 2014 mshitakiwa Nyamangaro alijilipa mishahara ya wafanyakazi hewa ya zaidi ya Sh. milioni 29.4 huku akijua wazi kwamba kitendo hicho ni kinyume na sheria.

Mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Joyce Minde, Ng’hoboko alidai kwamba mshitakiwa huyo alikuwa akijipatia mishahara hiyo ambayo wahusika waliisha staahafu kazi.

Hata hivyo, mshitakiwa Nyamangaro alikana kutenda makosa hayo yote 57 na hivyo kesi yake kuahirishwa hadi Jumatano itakapotajwa tena.

Wiki iliyopita, serikali ilitangaza kuanza uchunguzi kuwabaini watumishi wote waliokuwa wakijilipa mishahara ya wafanyakazi hewa ili hatimaye wachukuliwe hatua.

Kwa mujibu wa Waziri wa Utumishi, Angela Kairuki, watumishi hewa wameshaisababishia serikali hasara Sh. bilioni 7.6 kuanzia Januari hadi Machi.

Akihutubia wananchi wakati wa ufunguzi wa daraja la Nyerere, Kigamboni jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki, Rais Magufuli alisema kuna zaidi ya wafanyakazi hewa 7,700 ambao wameshagunduliwa mpaka sasa serikalini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post