WAZIRI WA MAMBO YA NJE AFUNGUKA KUHUSU MAREKANI KUINYIMA MSAADA TANZANIASerikali imeeleza kusikitishwa na uamuzi wa Marekani kusitisha uhusiano katika Shirika la Changamoto za Milenia (MCC), bila kuishirikisha wala kuisikiliza.Kadhalika, imesema hakuna umuhimu wa misaada ya afya na elimu inayofadhiliwa na Marekani kwa dola za Marekani milioni 700 (Sh. trilioni 1.5), kama imejitoa katika kusaidia miradi ya umeme ambayo ni muhimu katika utekelezaji wa miradi inayofadhili, kwa kuwa ni sawa na kutoa kwa mkono wa kulia na kupora kwa mkono wa kushoto.


Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, baada ya kupokea taarifa ya uamuzi wa MCC, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, alisema uhusiano na Marekani utaendelea katika maeneo mengine, lakini kwa fedha hizo hakuna la kufanya ingawa milango iko wazi iwapo watafikiria upya.


“Fedha ni zao, uamuzi ni wao wameutoa Washington. Hatuwezi kulia kwa ajili ya hili, tutaendeleza ushirikiano katika maeneo mengine, lakini tunawaomba wafanye uchambuzi wa kigezo cha demokrasia kwa asilimia 100 kinachotumika katika misaada hiyo,” alibainisha na kuongeza:


“Wametusaidia kwa miaka mitano kwa vile tulikidhi vigezo, ila sasa tumeshindwa kimoja inafuta imani na uelewano ambao ulikuwapo kati yetu. Nishati ndiyo nyenzo ya maendeleo kwa Tanzania. Kwa sasa tunaelekeza umeme vijijini ili vijana wanaosoma bure wajisomee na hospitali zitoe huduma muda wote.”


Waziri Mahiga alisema Tanzania imetia saini mkataba wa malengo ya milenia ambayo yanakwenda sambamba na MCC, hivyo kufuta fedha hizo kwa sasa ni sawa na kuumiza mahali panapouma zaidi huku ikiwa (Marekani) kiongozi wa utawala bora, demokrasia na soko huria duniani.


Alifananisha kunyimwa fedha hizo sawa na kutoa adhabu kwa mkosaji bila kujali kuwa alipaswa kumwelimisha na kumwonya kabla ya adhabu kubwa.


“Ukichukua mizani na kuweka nyama upande huu na jiwe upande mwingine, ukapima mazuri ambayo Tanzania imekuwa ikifanya na kuonekana mtoto mzuri machoni mwa dunia, lakini upungufu wa sasa waliouona, utaona tuna mazuri mengi, hivyo hatukustahili adhabu hii,” alisisitiza.


“Uamuzi wao hatuwezi kuwaingilia, nasi tukiamua yetu wasituingilie. Tumejitahidi tuwezavyo kulinda demokrasia na hatutarudi nyuma kwani katika uchaguzi wa Zanzibar vyama vilishirikishwa. Waelewe na kutambua mazuri yetu tunayofanya na tutaendelea kufanya,” afafanua.


Aidha, alisema suala la Zanzibar liliendeshwa vizuri kwa kuwa lilitoa nafasi ya mazunguzo kwa pande zote na kwamba hakuna mwenye uwezo wa kuingilia masuala ya uchaguzi, serikali na mambo ya ndani ya visiwa hivyo kwa kuwa wana katiba na sheria zao bali mambo machache tunashirikiana na hata Rais Dk. John Magufuli, alikuwa mwangalizi tu.


Balozi Mahiga aliishangaa Marekani kwa kueleza kuwa uamuzi wa sasa unapingana na tamko la hivi karibuni lililosisitiza mazungumzo baada ya serikali mpya kuingia madarakani, kwa kuwa kabla ya utekelezaji, imetoa uamuzi wa kuvunja uhusiano na Tanzania katika MCC.


“Kitu kinachoitwa demokrasia kingekuwa kinafugwa kwenye bomba na kuona kinamiminika ingekuwa rahisi sana, lakini ni kitu cha kulea na kutengeneza. Tanzania imejulikana duniani kama mlezi na mjenzi wa demokrasia tangu kipindi cha chama kimoja hadi vyama vingi,” alisema.


Aidha, alisema kutokana na hali hiyo, serikali itafanya marekebisho katika bajeti yake na mpango wa maendeleo ambao ulijumuisha fedha hizo na kwamba kinachopaswa kufanyika kwa sasa ni kujikita kwenye ukusanyaji wa kodi kikamilifu.


“Ndani ya vikao vya Bunge la Marekani tuna marafiki zetu ambao tunaamini wataendelea kuihoji serikali yao juu ya uamuzi huu na hasa wakizingatia historia yetu katika kukuza na kuendeleza demokrasia nchini,” alibainisha.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post