TANZANIA YAKOSA MAMILIONI KUTOKA SHIRIKA LA UFADHILI LA SERIKALI YA MAREKANI







Shirika la ufadhili la serikali ya Marekani limesitisha msaada wake kwa serikali ya Tanzania likilalamikia matukio kuhusu uchaguzi wa Zanzibar na kutekelezwa kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao.

Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) imesema Tanzania haijatimiza viwango vinavyohitajika ili kunufaika na ufadhili kutoka kwa shirika hilo, na hivyo basi haitapokea msaada wa awamu ya pili ambao ulikuwa wa jumla ya Dola 472.8 milioni ambazo ni sawa na shilingi trilioni moja za Tanzania.

Kupitia taarifa, bodi hiyo imesema: "Serikali ya Tanzania haijachukua hatua za kuhakikisha kuheshimiwa kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandao.”

Bodi hiyo aidha imesema Tanzania iliendelea na uchaguzi wa marudio Zanzibar ambao "haukushirikisha wote na wala haukuakisi maoni ya wote, licha ya malalamiko kutoka kwa serikali ya Marekani na jamii ya kimataifa.”

Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt Ali Mohammed Shein alitangazwa mshindi wa uchaguzi huo uliosusiwa na chama kikuu cha upinzani, Chama cha Wananchi (CUF).

MCC imesema kwamba huwa inatilia mkazo sana demokrasia na kujitolea kwa nchi kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.

"Uchaguzi uliofanyika Zanzibar na kutekelezwa nwa Sheria ya Uhalifu wa Mitandao vinaenda kinyume na hili,” imesema.

Tanzania ilipokea Dola 698 milioni katika awamu ya kwanza.

Pesa za MCC hutumiwa kufadhili miradi ya maji, barabara na nishati.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527