ACT WAZALENDO WATOA TAARIFA KUHUSU UAMUZI WA BODI YA WAKURUGENZI YA MCC WA KUSITISHA MAHUSIANO NA TANZANIATAARIFA KWA UMMA
UAMUZI WA BODI YA WAKURUGENZI YA MCC WA KUSITISHA MAHUSIANO NA TANZANIA YATAWAUMIZA WANANCHI WA VIJIJINI


CHAMA cha ACT-Wazalendo kimeupokea kwa masikitiko makubwa uamuzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa wa MCC wa kusisitisha mahusiano na Tanzania.


MCC ni Shirika la misaada la Marekani lilianzishwa na Bunge la Nchi hiyo mwaka 2004 kwa lengo la kusaidia miradi ya maendeleo katika nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa haraka wa uchumi.


Tangu kuanzishwa kwake, shirika hili limesaidia miradi mingi ya maendeleo nchini ikiwemo ujenzi wa barabarani na usambazaji wa umeme vijijini kwa sasa miradi ya aina hiyo inaendelea sehemu mbali mbali hapa nchini na miongoni mwao ni pamoja na mradi wa REA,miradi ya barabara kama ile ya Tnduma Sumbawanga pamoja na Tanga katika barabara ya Horohoro.


Pamoja na vigezo vingine, kigezo mama kwa nchi kufuzu kupata misaada ya MCC ni kwa nchi husika kuzingatia misingi kidemokrasia ikiwemo kufanya uchaguzi ulio huru na haki.


Jana tarehe 28 Machi 2016 Shirika la MCC lilitangaza kusitisha mahusiano na Tanzania kutokana na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM),kubariki kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika tarehe 25 Oktoba 205 na kubariki kurudiwa kwa uchaguzi huo tarehe 20 Machi 2016 katika mazingira ambayo hayakuzingatia misingi ya demokrasia ya vyama vingi na kuvunja matunda ya mwafaka wa kisiasa na kikatiba uliojengwa kwa gharama kubwa visiwani humo.


Chama cha ACT-Wazalendo kinapigania nchi yetu kujitegemea kiuchumi kama msingi wa kujenga utu na uhuru endelevu wa kisiasa na kijamii. Hata hivyo tunatambua kwamba katika kipindi hiki nchi yetu inahitaji mahusiano mema na Jumuiya ya Kimataifa na wadau mbalimbali wa maendeleo duniani, likiwemo shirika la MCC, katika kuendeleza miradi ya maendeleo. Shirika la MCC limekuwa mdau mkubwa katika miradi ya barabara na kusambaza umeme vijini.


Uamuzi huu wa Bodi ya Wakurugenzi wa MCC utawaumiza na kukwaza juhudi za wananchi wa vijijini katika kujikwamua na umaskini.


Tunasikitika kwamba ubabe wa Serikali ya CCM na woga wake wa kushindana kidemokrasia umesababisha nchi yetu ikose pesa za MCC ambazo zingesukuma mbele juhudi za kupambana na umaskini.


Tunatoa wito tena kwa Serikali ya chama cha Mapinduzi kuacha ubabe na kufifisha juhudi za miaka ishirini za ujenzi wa demokrasia hapa nchini. Tunatoa wito maalumu kwa wadau wote wa siasa visiwani Zanzibar kurudi mezani na kutatua mgogoro wa kisiasa kwa njia za kistaraabu na katika hali ambayo itarudisha heshima ya nchi yetu katika kukuza demokrasia nchini.


Imetolewa na


Theopister Kumwenda
Makamu Mwenyekiti, Kamati ya Katiba, Sheria na Mambo ya Nje
29/03/2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post