RAIS MAGUFULI ASHTUSHWA NA TAARIFA ZA MAALIM SEIF KUUGUA GHAFLA... AMTEMBELEA NA KUZUNGUMZA NAYE,ANGALIA PICHA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad jijini Dar es Salaam. Maalim Seif amemshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kumjulia hali na kusema kuwa hali yake ya kiafya inaimarika siku baada ya siku. 

*******
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtembelea na kumjulia hali Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Maalim Seif Shariff Hamad, katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es salaam, ambako anapata mapumziko baada ya kuruhusiwa kutoka hospitali ya Hindu Mandal alikokuwa amelzwa kwa matibabu.

Pamoja na kumpa mkono wa pole, Rais Magufuli amemuombea Maalim Seif Shariff Hamad kupona haraka ili aweze kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

"Nilishtushwa sana na taarifa za kuugua kwako, lakini sasa nafurahi kukuona ukiwa mwenye afya nzuri ikilinganishwa na taarifa nilizozipata hapo awali, nakupa pole sana" amesema Rais Magufuli wakati akimjulia hali hotelini hapo.

Kwa upande wake Maalim Seif Shariff Hamad amemshukuru Rais Magufuli kwa ukarimu na upendo aliouonesha kwa kumtembelea hotelini hapo, na amewahakikishia watanzania kuwa hali yake sasa inakwenda vizuri na inazidi kuimarika kila kukicha.

"Sasa hivi ninaweza kutembea vizuri, kufanya shughuli zote mwenyewe bila ya msaada wa mtu yeyote yule, na ni matumaini yangu kwamba baada ya muda mfupi, hali yangu itarudi kama kawaida, nije nishirikiane na watanzania wenzangu katika kutekeleza majukumu ya nchi yetu" Maalim Seif alimweleza Rais Magufuli.

Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es salaam
09 Machi, 2016.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF ambaye pia ni Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Shariff Hamad jijini Dar es Salaam mara baada ya kumjulia hali jijini Dar es Salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527