MZEE AKUTWA AMEFARIKI KWENYE CHOO CHA MSIKITI HUKO ZANZIBAR,YADAIWA ALIKUWA ANAVUA NGUO AOGE AKAANGUKA




MTU mmoja mwenye umri wa miaka 80 amekutwa akiwa amefariki ndani ya choo cha msikiti wa Ibadhi ulioko Bopwe karibu na Ofisi za Baraza la Wawakilishi Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba .


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini Kwake , Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Kamishina msaidizi Hassan Nassir Ali alisema aliyefikwa na mauti hayo ni Hassan Ali Juma mkazi wa Bopwe Wete .


Alisema mzee huyo aliondoka nyumbane kwake machi 9 majira ya saa saba , kuelekea msikitini kwa ajili ya maandalizi ya swala ya adhuhuri , na kuonekana machi 10 majira ya saa 12.45 jioni akiwa amefariki ndani ya choo .


Inadaiwa kuwa mzee huyo baada ya kufika msikitini aliingia chooni kisha kufunga mlango kwa ndani ambapo alianguka akiwa katika harakati za kufua fulana alilokuwa amevaa ili aoge.


“Tumebaini kwamba mzee huyo alianguka katika harakati za kuvua fulana , ambapo tumemkuta akiwa amefunikwa na fulana usoni huku akionekana kuumia zaidi sehemu za kichwani ”alifahamisha .


Akizungumza katika eneo la tukio Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa jeshi la Polisi Mkoa Issa Juma Suleiman aliwataka wananchi kutoa taarifa katika jeshi la Polisi wanapopotelewa na jamaa zao ili wasaidiane kuwatafuta .


Alieleza kwamba tangu mzee huyo alipopotea hakuna mtu aliyefika na kutoa taarifa katika jeshi la Polisi jambo ambalo ni kinyume na utaratibu .


Naye mdogo wa marehemu Khamis Ali Juma (42) alisema kabla ya kufikwa na mauti hayo kaka yake hakuwa na matatizo yoyote kiafya , na aliondoka nyumbani kwa ajili ya kuwahi swala ya Adhuhuri katika mskiti wa Ibadhi .


Mashuhuda wa tukio hilo walifahamisha baada ya kuona mlango umefungwa walichungulia na kumuoa akiwa amelala chini , ndipo juhudi za kuvunja zilichukuliwa chini ya usimamizi wa jeshi la Polisi .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527