MAAFISA WA TAKUKURU NA ASKARI POLISI WATAKA KUTWANGANA MAKONDE MAHAKAMANI HUKO GEITA
Maafisa wa Takukuru na askari wa Jeshi la Polisi waliokuwa wakilinda eneo la Mahakama ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, juzi nusura watwangane makonde wakati wakimgombea shahidi.


Tukio hilo lilianza kama masihara baada ya shahidi huyo kufika mahakamani akiongozana na maofisa wa Takukuru na ghafla mmoja wa polisi aliyemtambua, alimuweka chini ya ulinzi na kumfunga pingu.


Kamanda wa Takukuru wa wilaya hiyo, Chuzela Shija alilazimika kuingilia kati na kuwaomba polisi kumuachia mtu huyo, Paulo Sitephano ili atoe kwanza ushahidi ndipo hatua nyingine zifuate, ombi lililokubaliwa na polisi kwa kumfungua pingu huku wakimlinda asitoroke.


Sokomoko lilianza mara tu shahidi huyo alipomaliza kutoa ushahidi dhidi ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Umoja anayetuhumiwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh100, 000.


Polisi hao walimuwahi na kumfunga tena ili wampeleke kituoni. Kitendo hicho kiliwakera maofisa wa Takukuru ambao walitaka kuondoka na mashahidi wao wote watano walioenda nao mahakamani hapo kwa kutumia gari lao.


Maofisa hao wa Takukuru waliwasihi polisi kumuacha shahidi huyo na kuwataka wamkamate baada ya kukamilisha taratibu zao za kiofisi, ombi hilo lilikataliwa na askari hao.


“Hatuwezi kumuachia mtuhumiwa kwa sababu anatafutwa muda mrefu kwa tuhuma zilizofikishwa polisi,” alijibu mmoja wa polisi aliyekuwa na cheo cha sajenti ambaye alikataa kutaja jina lake.


Kitendo hicho kiliwakera maofisa wa Takukuru na kuamua kutumia nguvu kuwazuia polisi kuondoka na shahidi wao, hali iliyozua mtafaruku baina yao na kufikia hatua ya kukunjana mashati kabla ya kuamuliwa kuacha vitendo hivyo.


Baada ya vuta nikuvute na kurushiana maneno makali na vitisho, polisi walioongeza nguvu kwa kuita gari la doria, walifanikiwa kumchukua shahidi huyo na kumpandisha kwenye gari kabla ya kuondoka naye, huku maofisa wa Takukuru wakibaki kulalamikia ubabe wa askari hao.


Katika tukio hilo lililovuta watu wengi, baadhi ya maofisa wa Takukuru walionekana wana nguo zilizochanika, hali iliyosababishwa na mtafaruku huo.


Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa waendesha mashtaka wa polisi mahakamani hapo, Elias Mgobela aliwatupia lawama maofisa wa Takukuru kwa kushindwa kuonyesha ushirikiano kwa askari hao wakati wa kumtia mbaroni mtuhumiwa.


“Kisheria, polisi wana haki ya kumkamata mtuhumiwa eneo lolote. Huyo shahidi wa Takukuru alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu na polisi. Ilikuwa ni jukumu la maofisa wa Takukuru kushirikiana na polisi kufanikisha kumkamata badala ya kuzuia,” alisema.


Alisema kitendo hicho kilisababisha mmoja wa watuhumiwa aliyemtaja kwa jina moja la Lubango aliyekuwa chini ya ulinzi wa polisi kutoroka baada ya askari wengi kuelekeza nguvu kumgombea shahidi huyo.


Kwa upande wake, kamanda wa Takukuru wa wilaya, Chuzela Shija aliitupia lawama polisi akidai ilitumia ubabe, nguvu na dharau dhidi ya maofisa wake ambao hawakukataa shahidi wao kutiwa mbaroni, bali waliomba wapewe fursa ya kukamilisha taratibu za kiofisi kabla ya kumkabidhi mikononi mwao kwa tuhuma zinazomkabili.


“Isingewagharimu polisi kufuatana na maofisa wa Takukuru hadi ofisini, wakakamilisha taratibu za kiofisi na shahidi huyo, halafu wakamtia mbaroni. Ilihitajika busara ndogo sana kulimaliza suala hili, lakini bahati mbaya wenzetu walichagua kutumia ubabe na kutunishiana misuli,” alilalamika.


Katika kesi dhidi ya mwalimu huyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Amani Mwenegoha aliieleza mahakama jinsi alivyoshiriki kuweka mtego wa kumnasa.


Mkuu huyo wa wilaya alidai kuwa aliandaa mtego huo na kufanikiwa kumtia mbaroni mtuhumiwa huyo, Daniel Nying’ati baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mmoja wa wananchi aliyedai kuombwa fedha ili mtoto wake apate nafasi ya kurudia darasa la saba shuleni hapo.


Akiongozwa na mwendesha mashtaka wa Takukuru, Kelvin Murusuri, shahidi huyo alidai kuwa alichukua jukumu hilo kutekeleza moja ya majukumu yake ya kupokea, kusikiliza na kutatua kero za wananchi.


Alidai Februari 8, alipokea simu kutoka kwa mwananchi aliyemtaja kwa jina la Marko Elias akimtaarifu kuombwa rushwa na mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Umoja alipoenda kuomba nafasi ya mtoto wake kurudia darasa la saba shuleni hapo.


“Katika maelezo yake, mwananchi yule aliniambia aliombwa rushwa ya Sh150, 000, ndipo nilipomuambia aende Takukuru na kufanikisha mtuhumiwa kutiwa mbaroni,” alidai Mwenegoha.


Kwa upande wake, shahidi wa pili ambaye ni ofisa wa Takukuru, Redemta Miremi alidai Februari 8, alimpokea mwananchi aliyemtaja kwa jina la Marko Elias akidai kuelekezwa na mkuu wa wilaya kufika ofisi hizo kutoa taarifa ya kuombwa rushwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post