HAYA NDIYO MAZUNGUMZO YA RAIS MAGUFULI NA RAIS TROUNG TAN SANG WA VIETNAM IKULU JIJINI DAR ES SALAAM







Rais wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Mheshimiwa Truong Tan Sang ambaye amewasili hapa nchini jana jioni tarehe 08 Machi, 2016 kwa ziara ya kiserikali ya siku nne, amepokelewa rasmi na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Ikulu Jijini Dar es salaam.


Katika lango kuu lililopo Mashariki mwa Ikulu, Rais Truong Tan Sang amekagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na amepigiwa mizinga 21 iliyokwenda sambamba na nyimbo za mataifa yote mawili.


Pamoja na mapokezi hayo, Marais hao wawili wamefanya mazungumzo ya faragha ambayo yamehudhuriwa pia na makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, na baadaye kufuatiwa na mazungumzo rasmi kati ya Rais Magufuli na ujumbe wake na Rais Truong na Ujumbe wake.


Katika Mazungumzo hayo, Rais Magufuli ameahidi kuuendeleza na kuuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Vietnam ambao ulijengwa na waasisi wa mataifa haya mawili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Ho Chi Minh, hata kabla ya Uhuru, huku akitilia mkazo juu ya ushirikiano katika maendeleo ya kiuchumi.


Rais Magufuli amemweleza Rais Truong Tan Sang kuwa katika miaka mitano ijayo, Tanzania imedhamiria kujikita katika uanzishwaji wa viwanda vingi, na hivyo ametaka mahusiano kati ya Tanzania na Vietnam yajielekeze katika kuendeleza Kilimo na ufugaji na hivyo kuiwezesha nchi kuwa na uhakika wa chakula na pia kupata ziada itakayouzwa nchi.


"Tunatambua jinsi Vietnam ilivyopiga hatua kubwa katika uvuvi, uzalishaji wa kahawa na uzalishaji wa mpunga. Uzalishaji katika maeneo hayo umeiwezesha kuwa nchi inayoongoza duniani, na sisi Tanzania tunataka kujifunza kutoka kwenu" Amesisitiza Rais Magufuli.


Kufuatia hali hiyo, Rais Magufuli amemuomba Rais Truong Tan Sang, kuwa uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili ujikite katika kuendeleza kilimo hususani kutumia zana bora za kilimo badala ya jembe la mkono, Kilimo cha umwagiliaji badala ya kutegemea mvua, kuzingatia mbinu bora za ugani, kukabiliana na wadudu waharibifu wa mazao na kupata masoko ya mazao.


Kwa upande wake Rais wa Vietnam Mheshimiwa Truong Tan Sang amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa kuiongoza awamu ya Tano na amemhakikishia kuwa Vietnam itaendelea kushirikiana na Tanzania, huku ikitambua mchango mkubwa uliotolewa na watu wa Tanzania walioiunga mkono juhudi za kuiunganisha nchi hiyo na kuwa Jamhuri ya Kisoshalisti mwaka 1968.


Amesema kwa kuzingatia mazingira bora ya Tanzania yenye amani na utulivu, Vietnam imedhamiria kuwa Tanzania iwe kituo chake cha kuzifikia nchi nyingine za Afrika Mashariki na sehemu nyingine za Afrika.


Rais Truong Tan Sang ameomba mahusiano ya Tanzania na Vietnam, sasa yajielekeze katika kuongeza Biashara, huku akieleza kuwa biashara ya Dola za Marekani milioni takribani milioni 300 haitoshi, na hivyo amependekeza wafanyabiashara wa Tanzania kuunganishwa na wenzao wa Vietnam ili mauzo ya bidhaa kutoka pande zote mbili yaongezeke hadi kufikia dola za Marekani bilioni 1 ifikapo mwaka 2020.


Ameongeza kuwa Vietnam ipo tayari kutiliana saini mikataba mbalimbali ya ushirikiano katika biashara, Viwanda na Kilimo, na ametoa mwaliko kwa wakulima wa Tanzania kwenda kujifunza nchini Vietnam.


Mara baada ya Mazungumzo hayo, Marais wote wawili wamezungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari ambapo wote wawili wamesisitiza kuwa, nchi zao zipo tayari kukuza zaidi mahusiano na ushirikiano kwa faida ya wananchi wake.


Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam-09 Machi, 2016.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527