HAWA NDIYO MAWAZIRI WANAOWEZA KUTUMBULIWA MAJIPU NA RAIS MAGUFULI

Siku 87 tangu Rais John Magufuli awaapishe, mawaziri watano wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Awamu ya Tano wako kwenye msukosuko kutokana na kutajwa, kuhusishwa ama kufanya uamuzi wenye dalili za majipu.


Mawaziri hao, George Simbachawene, Profesa Sospeter Muhongo, Jenister Mhagama, Harison Mwakyembe na January Makamba wamekuwa wakihusishwa na kufanya uamuzi bila ya kufuata kanuni, kufanya mipango ya kuwezesha mgeni kupata zabuni za ujenzi, kufanya uteuzi kinyume na taratibu na kustua watendaji wajiandae kukabiliana na ziara za kustukiza za viongozi wakuu wa Serikali.


Rais John Magufuli, ambaye amekuwa akiwawajibisha watendaji wa umma tangu aapishwe Novemba 5, 2015, alishasema kuwa hataonea aibu yeyote atakayeonekana kutokwenda na kasi yake, msimamo unaowaweka mawaziri hao kwenye hali ngumu wakati huu ambao tuhuma dhidi yao zinashamiri.


Hadi sasa, Serikali haijatoa tamko kuhusu tuhuma zilizoibuliwa dhidi yao, wakati Rais amekuwa hatabiriki katika uamuzi wake na hali hiyo aliizidisha Jumapili alipomuondoa Ombeni Sefue siku 67 baada ya kumteua tena kuendelea na nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi.


Simbachawene, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) amekuwa akitajwa kwenye sakata la ununuzi wa mafuta ya mwezi Septemba, Oktoba na Novemba mwaka 2015 bila ya kushindanisha zabuni na hivyo kusababisha aliyepewa kazi hiyo kupandisha bei kwa Sh40 bilioni.


Mbunge huyo wa Mpwapwa, ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, alijitetea kuwa alichukua uamuzi huo kutokana na wasiwasi wa usalama baada ya Uchaguzi Mkuu na sheria inamruhusu kufanya hivyo.


Hata hivyo, Ewura ilisema wakati Waziri Simbachawene anafikia uamuzi huo tayari kulikuwa na zabuni mezani na walitoa ushauri wao.


Ewura ilisema ununuzi huo umesababisha bei ya mafuta kutoshuka kwa kadiri inavyotakiwa na hivyo kuwafanya Watanzania wasinufaike na kuporomoka kwa bei ya nishati hiyo duniani.


Profesa Muhongo anatajwa kuhusika katika sakata la uwashwaji wa mita ya kupimia mafuta kwenye Bandari ya Dar es Salaam siku moja kabla Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutembelea eneo hilo.


Mita hizo zilikuwa zimezimwa kwa takriban miaka mitano kwa madai kuwa ilikuwa ikipunja wafanyabiashara, lakini iliwashwa kabla ya ziara hiyo baada ya Profesa Muhongo kudaiwa kumtaka bosi wa Wakala wa Vipimo, Magdalena Chuwa kuziwasha siku moja kabla ya ziara ya Majaliwa.


“Mita imeanza kufanya kazi jana kutokana na maagizo yaliyotolewa ngazi za juu, nilitumiwa meseji (ujumbe mfupi) kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo.Aliagiza ianze kazi ndani ya saa 24,” alisema Chuwa alipoulizwa na Majaliwa kuhusu kuwaka kwa mita hizo.


Kwa nyakati tofauti, Profesa Muhongo amelitolea ufafanuzi suala hilo akisema kuwa mita hizo zinamilikiwa na wakala wa vipimo ambao uko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.


Waziri mwingine, Mhagama ambaye anaongoza Wizara ya Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, alifanya uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk Carina Wangwe, lakini saa tano baadaye alilazimika kutengua “kutokana na kutokamilika kwa baadhi ya taratibu”.


Nafasi ya bosi huyo NSSF imezingirwa na mbigiri na hadi sasa haijapata mrithi wala kaimu wake. Dk Wangwe, ambaye ni Mkurugenzi wa Tehama wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Hifadhi ya Jamii (SSRA), aliteuliwa kushika nafasi hiyo Machi 3 saa 11:15 jioni na kutenguliwa siku hiyo hiyo saa 4:15 usiku.


Aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alitolea ufafanuzi suala hilo kwamba uteuzi huo ulikosewa na Dk Wangwe aliteuliwa kuwa mwangalizi tu, siyo kaimu mkurugenzi mkuu.


“Kiswahili cha neno caretaker (mwangalizi) kilikosewa na kuandikwa kaimu mkurugenzi mkuu na hiyo imetokea wakati ambao taratibu za kupata kaimu hazijakamilika.Kutokana na mkanganyiko huo, waziri aliamua kutengua tu,” alisema Balozi Sefue.


Sakata jingine linamuhusisha January, ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais.


Waziri huyo kijana anatajwa kwenye tuhuma zinazomuhusisha dada yake, Mwamvita za mipango ya kumtafutia zabuni raia wa Italia, Vincenzo Cozzolino kwa kutumia nafasi za kisiasa. Zabuni niyo ni ya ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, ambao umesimamishwa kwa muda kutafuta fedha.


Tuhuma hizo zimetanda kwenye baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya jamii, ingawa wawili hao wamekanusha kuhusika lakini wanakiri kuwapo kwa uhusiano baina ya Mwamvita na Cozzolino uliohusisha kupeana fedha.


January alisema kuwa raia huyo wa Italia alikuwa na urafiki na dada yake, lakini anashangazwa na kitendo cha kutajwa jina lake katika suala hilo.


Cozzolino amenukuliwa katika vyombo vya habari akikanusha January kuhusika katika suala hilo, huku katika mitandao ya kijamii kukiwa na taarifa zinazoonyesha mawasiliano kati ya Mwamvita na raia huyo wa Italia.


Chanzo cha taarifa hizo ni sauti za mazungumzo baina ya Cozzolino na Mwamvita zilizorekodiwa kupitia akaunti ya Instagram ya mmoja wa watu wanaomfahamu Mwamvita, kisha kusambazwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.


January pia yumo kwenye sakata la mawaziri watano walioshindwa kujaza fomu za mali wanazomiliki lililobainika Februari 25, mwaka huu.


Kwa upande wake Dr Mwakyembe,anatuhumiwa akiwa Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, wizara yake iliingiza mabehewa feki 25 na kuisababishia serikali hasara ya mamilioni ya pesa. Sakata hilo la mabehewa limewafikisha baadhi ya watumishi mahakamani

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post