NCHI 10 ZATANGAZA KUSITISHA UFADHILI WAO TANZANIA



Nchi 10 kati ya 14 za umoja wa Ulaya zimetangaza kusitisha ufadhili wao kwa bajeti ya serikali ya Tanzania.



Nchi hizo, zikiwemo Sweden na Ireland, zimechukua hatua hiyo siku chache baada ya shirika la utoaji misaada la serikali ya marekani (MCC) kuondoa msaada wa dola 472 wa kufadhili miradi ya maendeleo kwa Tanzania.

Bodi ya MCC ilisema hatua yake ilitokana na mzozo kuhusu uchaguzi wa kisiwa cha Zanzibar na utekelezwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandao.

Mataifa yaliyositisha ufadhili wao kwa bajeti ya Tanzania hata hivyo hayajaeleza sababu ya kufanya hivyo.

Ubalozi wa Sweden umethibitisha kwamba taifa hilo limesitisha ufadhili wake kwa bajeti ya Tanzania, lakini ukasisitiza kwamba hatua hiyo haihusiani na yaliyojiri katika uchaguzi wa visiwa vya Zanzibar.

"Mwaka uliopita, Sweden ilikuwa moja ya nchi zilizositisha ufadhili wake kwa bajeti ya Tanzania kutokana na tuhuma za ufisadi kuhusiana na sekta ya kawi [na mkataba wetu na serikali ulifika kikomo mwaka jana],” ubalozi huo umeambia BBC.

“ Sweden inafurahishwa na juhudi za serikali kukabiliana na ufisadi na iko tayari kuanzisha majadiliano na serikali ya Tanzania na wafadhili wengine kuhusu mikakati ya kufadhili bajeti ya Tanzania siku zijazo.”

Ubalozi wa Ireland pia umethibitisha kwamba ni kweli taifa hilo halifadhili tena bajeti ya Tanzania.

Ufadhili wake wa mwisho ulitolewa mwaka wa kifedha wa 14/15, malipo ambayo yalifanyika Juni 2015 na kwa sasa hakuna malipo yaliyoratibiwa ya mwaka wa kifedha wa 15/16.

"Mpango ulimalizika Juni 2015 na hakuna mipango mingine ya kutoa ufadhili kwa bajeti (ya Tanzania),” ubalozi wa nchi hiyo umesema.

Karibu theluthi moja ya bajeti ya Tanzania ilitegemea msaada mwaka uliopita, kwa hivyo hatua ya nchi hizo ni pigo kwa mipango ya maendeleo ya serikali mpya.
Chanzo: BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527