Ushirikina Kahama !! MAMA AUAWA KWA KUPIGWA MCHI WA KUTWANGIA BAADA YA MTOTO WAKE KUKATWA UUME WAKE



Mwanamke aliyejulikana kwa jina la Ester Misalaba(19) ameuawa kwa kupigwa utosini kwa mchi wa kutwangia na mke mwenza aliyemtuhumu kukata uume wa mtoto wake Frank Bahati mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi kutokana na imani za kishirikina.

AKitoa taarifa kwa vyombo vya habari,kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Mika Nyange alisema tukio hilo limetokea juzi saa 10 jioni katika kijiji cha Mlinza,kata ya Bugomela wilayani Kahama.

Akisimulia tukio kamanda Nyange alisema Ester Misalaba(19) mkazi wa Mulinza D aliuawa kwa kupigwa kichwani na mchi wa kutwangia na Mariam Hamis(26) ambaye ni mke mwenza na kusababisha kifo chake papo hapo.

“Chanzo cha tukio hili ni imani za kishirikina baada ya Mariam Hamis kumkata ngozi ya uume mtoto wa mke mwenzie Ester Misalaba aitwaye Frank Bahati mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili kisha Mariam Hamis kuondoka na ngozi hiyo ya uume wa mtoto”,alieleza Kamanda Nyange.

“Mama mwenye mtoto Ester Misalaba alipogundua kuwa mwanaye katolewa ngozi ya uume,ndipo ugomvi ulipoanza kati yao,mtuhumiwa(Mariam Hamis) akachukua mchi na kumpiga marehemu katikati ya utosi na kufariki dunia papo hapo,bado tunachunguza tukio hili”,aliongeza Kamanda Nyange.

Wakati huo huo mkazi wa kijiji cha Mwasaligula kata ya Lyabusalu wilaya ya Shinyanga Mazengea Kazungu (49) amevamiwa akiwa nyumbani kwake na watu watatu wasiofahamika waliokuwa na silaha inayodhaniwa kuwa ni SMG kwa lengo la kupora pesa.

Kamanda Nyange alisema tukio hilo limetokea juzi saa 1:30 usiku ambapo watu hao walivamia nyumba ya Kazungu kisha kufyatua risasi moja hewani na kujaribu kupora lakini hawakufanikiwa kutokana na kelele za wakazi wa eneo hilo.

Alisema juhudi za kuwabaini na kuwakamata wahusika wa tukio hilo zinaendelea. 
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527