TUME YA VYUO VIKUU TANZANIA -TCU YAFUTA CHUO CHA MTAKATIFU YOSEFU TANZANIA KAMPASI YA ARUSHA


1.Tunapenda kuuarifu umma kwamba, Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania (SJUIT) Kampasi ya Arusha ni mojawapo ya vyuo vikuu vilivyosajiliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) ambacho kilianza kudahili wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka wa masomo 2013/2014.




2.Kwa mujibu wa kifungu cha 5(1) cha Sheria ya Vyuo Vikuu, Sura ya 346 ya Sheria za Tanzania, Tume ina mamlaka ya kusimamia na kudhibiti ubora na usimamizi wa uendeshaji wa Vyuo Vikuu hapa nchini.


3.Kwa muda mrefu na kwa wakati tofauti kumekuwapo na matukio ya migogoro baina ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Kampasi ya Arusha na wanafunzi.


Kwa kipindi hiki chote Tume imekuwa ikifuatilia kwa karibu chimbuko la migogoro hiyo na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kutoa maelekezo kwa uongozi wa chuo kurekebisha kasoro zinazosababisha migogoro chuoni hapo.


Kwa sehemu kubwa migogoro hiyo imekuwa ikitokana na matatizo ya ubora, uongozi, ukiukwaji wa sheria na taratibu za uendeshaji wa chuo kikuu kama zilivyobainishwa na Sheria ya Vyuo Vikuu.


Hata hivyo jitihada za Tume ya Vyuo Vikuu kukitaka Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania (SJUIT) Kampasi ya Arusha kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa katika Kampasi hii inakidhi viwango vya ubora vilivyowekwa na Tume hazikupewa uzito stahiki na uongozi wa chuo.


4.Hivi sasa Kampasi ya Arusha ina jumla ya wanafunzi 1557 wanaosoma programu za masomo ya ualimu wa sayansi zifuatazo:


5.Kutokana na yaliyobainishwa hapo awali, tunapenda kuuarifu umma kwamba, Tume imejiridhisha kuwa Kampasi ya Arusha ya Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania imepoteza sifa na vigezo vya kuendelea kutoa elimu ya chuo kikuu.


Kwa kuzingatia ukweli kwamba wanafunzi ndio waathirika wakuu wa matatizo yaliyopo kwenye Kampasi hii, Tume imeamua kama ifuatavyo:


a)Imefuta kibali kilichoanzisha Kampasi ya Arusha ya Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Tanzania (SJUIT) na kuidhinisha uhamisho wa wanafunzi wote waliokuwa wanasoma katika Kampasi hiyo ya Arusha kwa gharama za Chuo Kikuu cha SJUIT. Orodha ya majina yao na vyuo watakavyopangiwa itatangazwa na kuwekwa katika tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu hivi punde.


b)Imefuta udahili wa wanafunzi wapya katika programu ya shahada ya miaka mitano ya ualimu wa sayansi. Na kwamba, wanafunzi wanaoendelea na masomo katika programu hii watahamishiwa katika Kampasi ya Luguruni, Dar es Salaam, na watalazimika kwanza kuhitimu katika ngazi ya Stashada (Diploma) kama ilivyokuwa imeidhinishwa na Tume hapo awali. Utaratibu wa uhamisho wa wanafunzi wa programu hii utatangazwa hivi punde na kuwekwa katika tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu.


c) Imeidhinisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza ambao hawakuweza kupata udahili katika vyuo vikuu vingine, kutoka katika kundi la wapatao 500 waliofukuzwa chuoni kutokana na migogoro iliyojitokeza katika Kampasi ya Arusha mwezi Juni, 2015 kuendelea na masomo katika vyuo watakavyopangiwa baada ya taratibu za uchambuzi wa taarifa zao kukamilika. Orodha ya majina yao na vyuo watakavyopangiwa itatangazwa na kuwekwa katika tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu hivi punde.


6.Kufuatia uamuzi huu, wanafunzi wote wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Mt. Yosefu Kampasi ya Arusha wanaarifiwa kuwa watahamishiwa kwenye vyuo vikuu vingine vinavyofundisha programu za masomo zinazofanana na masomo wanayosoma hivi sasa chini ya utaratibu na masharti yafuatayo:


i)Wanafunzi wote wanapaswa kuondoka chuoni mara moja baada ya kukamilisha taratibu za kukabidhi mali na vifaa vingine vya chuo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.


ii)Wanafunzi wote wanatakiwa kuripoti kwenye vyuo watakavyopangiwa wakati wa kufunguliwa kwa muhula (semester) wa pili. Tarehe halisi ya kuanza kwa muhula wa pili kwa kila chuo watakachopangiwa itatangazwa na kuwekwa kwenye tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.


iii)Wanafunzi wanaosoma shahada ya miaka mitatu ya ualimu wa sayansi katika masomo yafuatayo watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM):

a)Bachelor of Science in Education with Mathematics & Chemistry;

b)Bachelor of Science in Education with Physics & Chemistry, na

c)Bachelor of Science in Education with Physics & Computer Science.


iv)Wanafunzi wanaosoma shahada ya miaka mitatu ya ualimu wa sayansi na Kompyuta (Bachelor of Science in Education with Mathematics & Computer Science) watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (RUCU):


v)Wanafunzi wanaosoma shahada ya miaka mitatu ya ualimu wa sayansi katika masomo yafuatayo watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU):

a)Bachelor of Science in Education with Physics & Mathematics; na

b)Bachelor of Science in Education with Biology & Chemistry.

vi)Orodha ya wanafunzi waliohamishwa na majina ya vyuo vikuu walivyohamishiwa itatangazwa na kuwekwa kwenye tovuti ya Tume ya Vyuo Vikuu hivi punde.


vii)Wanafunzi wote waliohamishwa ambao hawakukamilisha mitihani yao ya mwisho wa muhula wa kwanza, au hawakufanya kabisa mitihani hiyo, watatakiwa kufanya mitihani hiyo katika vyuo vikuu watavyohamishiwa kwa utaratibu maalum utakaondaliwa na chuo husika.


viii) Kila mwanafunzi anawajibika kutunza kumbukumbu zake zote muhimu za maendeleo ya kitaalama kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ikiwa ni pamoja na matokeo ya mitihani aliyokwishafanya.


ix)Wanafunzi wote ambao ni wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, mikopo yao itahamishiwa katika vyuo wakapokuwa wamehamishiwa.


7.Kampasi nyingine za Chuo Kikuu cha SJUIT (Luguruni na Boko – Dar es Salaam; na Makambako – Njombe) zitaendelea na masomo kama kawaida.


8.Kwa taarifa hii, vyuo vikuu vyote nchini vinakumbushwa kufuata sheria na kuzingatia utoaji wa elimu inayokidhi viwango vya ubora vinavyokubalika kitaifa na kimataifa. Tume haitasita kuchukua hatua stahiki kwa chuo kikuu chochote kitakachobainika kutoa elimu isiyokidhi viwango vya ubora kwa kisingizio cha aina yoyote.

Imetolewa na


PROF. YUNUS D. MGAYA

Katibu Mtendaji

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
26 Februari 2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527