MAWAZIRI WATEKELEZA AGIZO LA RAIS MAGUFULI KUJAZA TAMKO LA RASILIMALI NA MADENI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema agizo lilitolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli la kuwataka mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni wakamilishe kabla ya saa 12 leo jioni limetekelezwa.


Waziri Mkuu amepokea barua kutoka kwa Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji (Mst.) Salome Kaganda ikithibitisha kuwa mawaziri na naibu mawaziri wote wametekeleza agizo hilo.


“Hadi kufikia saa 9.30 leo alasiri (Ijumaa, Februari 26, 2016) mawaziri wote walikuwa wamekamilisha fomu zao za kuzikabidhi katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,” alisema Waziri Mkuu.


Rais Magufuli leo asubuhi alitoa maelekezo kwamba Mawaziri ambao hawajajaza Tamko la Rasilimali na Madeni ifikapo leo Ijumaa tarehe 26 Februari, 2016 saa 12.00 jioni wawe wamejaza na kurejesha Fomu ya Tamko la Rasilimali na Madeni katika Ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Dar es Salaam. Waziri ambaye atashindwa kutekeleza agizo hili atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake.


Mawaziri waliotakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilimali pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Charles Kitwanga na Waziri wa Nchi (OMR – Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba.

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga ambaye alitakiwa kurejesha hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako ambaye alitakiwa kutoa tamko la rasilmali na madeni.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi (OMR – Mazingira), Mhe. Luhaga Mpina alitakiwa kurejesha fomu za tamko la rasilmali na madeni pamoja na hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,11410 DAR ES SALAAM.
IJUMAA, FEBRUARI 26, 2016

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post