MZIMU WA MADARAKA WAIGUBIKA TAKUKURU,KILA MMOJA ANATAKA KUPANDISHWA CHEOMGOGORO wa ndani unafukuta katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU), Ofisi za Makao Makuu, baada ya baadhi ya watumishi kupandishwa vyeo bila kufuata utaratibu.

Taarifa za uhakika kutoka taasisi hiyo nyeti nchini, zimesema upandishwaji huo holela ulifanywa wakati wa uongozi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu, Dk. Edward Hosea.

Inadaiwa mtekelezaji alikuwa Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Ekwabi Mujungu.

Mujungu na wenzake watatu walisimamishwa kazi baada ya kukiuka agizo la Rais John Magufuli, linalowataka watendaji wa Serikali kutosafiri nje ya nchi hadi wapate kibali kutoka Ofisi ya Rais.

Vyanzo vya habari ndani ya TAKUKURU vimesema kwa mujibu utaratibu, kabla ya mfanyakazi kupandishwa cheo, kikao maalumu cha wakurugenzi kiitwacho KAWI hukaa na kutoa uamuzi wa kuwapandisha vyeo wafanyakazi kwa kuangalia vigezo vya utendaji.

“Kuna wenzetu kadhaa ambao wamepandishwa vyeo hapa kwetu bila taratibu kufuatwa, jambo ambalo limeathiri kwa kiasi kikubwa ari ya utendaji kazi kwa sababu kuna baadhi ya wafanyakazi ambao wanatekeleza majukumu yao kwa weledi mkubwa lakini wameachwa.

“Unakuta mtu ana miaka minne kazini lakini hajawahi kusimamia kesi mahakamani akashinda, lakini anapandishwa cheo na ngazi ya mshahara na kulingana mtu aliyefanya kazi kwa miaka 11,” kilisema chanzo chetu.

Baadhi ya majina ya watumishi ambao wamepanda vyeo na ngazi za mshahara au (BSS) katika mabano, kinyume cha utaratibu ni Lilian William (kutoka BSS I hadi BSS III), Ally Feo (BSS I hadi IV), Bruno Mchopa (BSS I hadi BSS IV).Wengine ni Tunu Mlele (BSS I hadi BSS IV), Malimi Magembe (BSS III hadi ABS ambayo ni ngazi ya juu ya mshahara) na Pendo Sagati (BSS I hadi BSS III).

Alipoulizwa kuhusu suala hilo siku kadhaa zilizopita, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Danietta Tindamanyire, alikataa kulizungumzia na kusema yeye si msemaji wa taasisi hiyo.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Valentino Mlowola, hakukiri kufahamu suala hilo wala kukanusha.

Alisema; “Kama mnazo hizo taarifa basi tuandikieni, tutafanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki mara moja.”

Wafanyakazi kadhaa wa TAKUKURU Makao Makuu ambao walizungumza na Mtanzania walisema upungufu katika Kurugenzi ya Utawala na Rasilimali Watu kwa kiasi fulani unachangiwa na wanaoongoza idara hiyo muhimu kutokuwa na taaluma husika ya masuala ya utawala na rasilimali watu.

Wakitoa mifano pamoja na vielelezo, walisema Mkurugenzi aliyesimamishwa (Ekwabi Mujungu) kitaaluma ni Ofisa Mipango, ambaye alipata elimu yake katika Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro.

Pia Kaimu Mkurugenzi wa sasa, Danietta Tindamanyire, naye pia hana taaluma husika.

Inelezwa kuwa vyeti vyake vinaonyesha kuwa kati ya Juni na Desemba, 1995, alisoma masomo ya kompyuta ngazi ya diploma katika chuo kiitwacho First Computers, India.

Kuanzia Januari hadi Julai 1997, alisoma na kupata cheti katika masuala ya fedha kutoka chuo hicho hicho, ambako Agosti mwaka huo huo alihitimu shahada ya kwanza (Bachelor of Arts) kutoka Chuo Kikuu cha Mohanlal Sukhadia, Udaipur, India.

Mwaka 2006 hadi 2009 alisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kupata Shahada ya Uzamili katika masuala ya Uchumi (Masters of Arts-Economics).

Taarifa zaidi zimesema tayari malalamiko ya wafanyakazi kuhusu upendeleo katika kupandishwa vyeo yamekwisha kumfikia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Angela Kairuki, ambaye ameahidi kuyafanyia kazi.
Via>>

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post