KINARA WA UJAMBAZI MBAGALA AKAMATWA ,WASHIRIKA WAKE WANASWA WAKIFUNGA NDOA MSIKITINIKamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro.
Siku nne baada ya majambazi 12 kuvamia Benki ya Access tawi la Mbagala, jijini Dar es Salaam na kuiba Sh. milioni 20 na kusababisha vifo vya watu sita, mtu anayedaiwa kuwa kinara wa uhalifu huo ametiwa mbaroni baada ya kutajwa na washirika wake, akiwamo aliyekamatwa akiwa anafunga ndoa.

Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa, kinara wa ujambazi huo alikamatiwa Sinza Mori, wilaya ya Kinondoni jana, saa 11:00 jioni.Kwa mujibu wa taarifa ambazo Nipashe ilizipata, kikosi kinachoshirikisha askari wa majeshi mbalimbali ikiwamo, polisi na la wananchi wa Tanzania, kilinasa watu wanne kwenye sherehe ya harusi baada ya kufuatilia mawasiliano yao ya simu.“Unajua sasa hivi hili suala linahusisha jeshi ambao wamefuatilia kwenye mtandao na kunasa simu za watu wanne ambao wamekamatwa huko Mbagala, akiwamo bwana harusi na watu wengine wanne,” kilisema chanzo chetu.Taarifa hizo zinasema baada ya watu hao kukamatiwa wakiwa wanafunga ndoa msikitini, walisaidia kutoa taarifa ambazo hatimaye zilifanikisha kukamatwa kwa mtu huyo anayedaiwa kuwa ni kinara wa ujambazi huo.Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alipoulizwa kuhusu tarifa hizo alisema bado hajazipata na kwamba yawezekana wasaidizi wake wamemkamata lakini bado hawajamfikishia taarifa.“Sina chochote hadi sasa ningekuwa nacho kwa nini nikunyime wakati ni jambo la sifa kwetu,” alisema Kamanda Sirro.Kinara huyo amekamatwa ikiwa imepita siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kutangaza uwezekano wa kutumia Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kushirikiana na polisi kuwasaka wahalifu wote waliojificha kwenye misitu ya Bagamoyo na Pwani, ambako inadaiwa walikimbilia baada ya tukio la Mbagala.Pia waziri huyo alisema katika operesheni hiyo, watakuwa wakiwasimamisha mara kwa mara watumia pikipiki kwa sababu vyombo hivyo vimekuwa vikitumiwa na majambazi katika kufanikisha matukio yao.TUKIO LILIVYOKUWA

Juzi Kamanda Sirro alisema majambazi hao wakiwa na silaha aina ya SMG na mabomu matatu ya kutupa kwa mkono yaliyotengenezewa Russia, walifika kwenye benki ya Access tawi la Mbagala wakiwa na pikipiki sita.Alisema kila pikipiki ilikuwa na majambazi wawili na baada ya kuwasili eneo hilo walishambulia polisi waliokuwa nje wakilinda benki hiyo.“Walivamia chumba cha askari nje ya benki na kumuua kwa kumpiga risasi kichwani askari wetu na kumjeruhi mwingine eneo la maungoni, kisha kuchukua silaha na kuingia ndani ya benki,” alisema.Alisema baada ya kuingia ndani, walimshambulia mlinzi binafsi wa kampuni ya ulinzi ya Security Group of Afrika, Baraka Fredrick maarufu kama Selemia, ambaye alifariki papo hapo.Pia alisema majambazi hao waliwashambulia na kuwajeruhi kwa risasi wafanyakazi wawili wa benki hiyo ambao ni Ofisa Mikopo, Salum Juma na Francis Amani waliokuwa chumba cha kuhifadhia fedha (Strong Room).“Walipiga ‘Safe’ yakuhifadhia fedha lakini haikufunguka ndipo wakaamua kwenda kaunta na kufanikiwa kupata Sh. milioni 20 na kuondoka nazo,” alisema.Alisema wakati wanaondoka walifyatua risasi iliyompata kidevuni Abdi Salum maarufu kama Shemdoe ambaye ni muuza duka jirani na benki hiyo.Kamanda Sirro alisema jeshi la polisi lilikuwa limejiimarisha kiulinzi maeneo hayo, vikiwamo vikosi vya farasi , pikipiki na magari, walianza kuwafuatilia majambazi hao ambao wakati huo walikuwa wakitumia usafiri wa pikipiki.Alisema katika majibizano ya risasi polisi waliwaua majambazi watatu na kufanikiwa kupata SMG tatu na pikipiki sita.Alisema majambazi wengine walikimbia kwa miguu na kuziacha pikipiki hizo, lakini fedha zilizoibwa hawakufanikiwa kuzipata.Kamanda Sirro alisema vikosi vyake viliendelea kuwafukuza majambazi wengine hadi msitu wa Kongowe unaotokea mkoa wa Pwani.

“Majambazi hao walitokomea ndani ya msitu huo na polisi tunaendelea kuwasaka na tunaahidi kuwakamata,” alisema.


Aliongeza kuwa, walishindwa kuwapiga risasi wakati wakiwakimbiza kwa kuhofia kujeruhi wananchi wengi waliokuwa eneo hilo.


“Ili kuonyesha majambazi hawa walikuwa wamejipanga, walitumia mbinu ya kivita kwa kuvamia wakiwa na mabomu ili waliovamiwa wasipate msaada, askari wetu aliyejeruhiwa ambaye amelazwa Muhimbili alifanya kazi kubwa licha ya majeraha aliyopata,” alisema.

CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527