Balaa Katavi !! WANANDOA WAUA MTOTO WAO KISHA MWILI KUUFUNGIA CHUMBANI SIKU TATU,WANANZENGO WAANZISHA TIMBWILI LA HATARI




Wanandoa wawili Juma Seleman (28) na Suzana Elias (24) wakazi wa Mtaa wa mji wa Zamani Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi wamesurika kifo kutoka kwa kundi la wananchi waliotaka kuwaua kwa kuchoma moto nyumba waliokuwa wakiishi.


 
 Wananchi hao walikasirishwa na kitendo cha wanandoa hao kumuua mtoto wao Justina Laurent (3) kwa kumchoma na moto kichwani na mikononi na kisha kuuficha mwili wa marehemu ndani ya chumba walichokuwa wakiishi kwa muda wa siku tatu.

Tukio hilo la kusikitisha la mauaji ya mtoto huyo lilitokea  jana majira ya saa moja na nusu usiku katika mtaa huo wa mji wa zamani mjini Mpanda na kuhuzunisha mamia ya wakazi wa Manispaa ya mji wa Mpanda

Mwenyekiti wa Mtaa huo Magreth John aliiambia Malunde1 blog  kuwa alipata taarifa za kuuawa kwa mtoto huyo ambaye alikuwa akiishi na baba wake wa kambo aliyekuwa amemuoa mama yake Suzana Elias.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo kutoka kwa wapangaji wa nyumba hiyo alifika kwenye nyumba hiyo na ndipo walipomweleza kuwa kuna mtoto ameuawa na wazazi wake na wamemfungia ndani wakiwa wameuficha mwili huo wa marehemu kwa muda wa siku tatu .

Mwenyekiti huyo wa mtaa alieleza kuwa wapangaji hao walishtushwa baada ya kubaini mtoto huyo kutoonekana kwake kwa muda wa siku tatu na chumba walichokuwa wakiishi wanandoa hao kuanza kutoa harufu ya kitu kilicho oza na kila walipoulizwa mtoto wao yuko wapi wanandoa hao walionekana kuwa na mashaka na walijibu kuwa mtoto wao anaumwa.
 
Alisema ndipo wapangaji walipoamua kutoa taarifa kwa mjumbe wa serikali ya mtaa Martha Idd ambaye naye alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa mtaa ambaye alitoa taarifa jeshi la Polisi na waandishi wa habari .

Polisi walifika kwenye eneo hilo na kukuta kundi la watu huku wakiwa na silaha za jadi mawe na fimbo wakiwa wameizingira nyumba hiyo kwa lengo la kutaka kuwashambulia wanandoa huku wengine wakiwa wamebeba mafuta ya taa kwa lengo la kutaka kuchoma nyumba hiyo .

Askari polisi ambao walikuwa na silaha za moto walifanikiwa kuwatawanya wananchi hao na kisha waliingia ndani ya chumba na kuwachukua wanandoa hao wawili na kuwapeleka kituo cha polisi cha Mpanda mjini huku wananchi hao wakiwasindikiza kwa kuwarushia mawe.

Hata hivyo polisi waliokuwa wamebaki hapo pamoja na mwenyekiti wa mtaa walifanya uchunguzi wa awali wa kuukagua mwili wa marehemu mtoto huyo na waliukuta ukiwa umechomwa na moto kichwani na mikononi huku ukiwa umeanza kuharibika na ukiwa unatoa maji.

Mmoja wakazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina la Maria Komba alieleza kuwa kabla ya tukio hilo amekuwa akisuluhisha ugomvi wa mara kwa mara  wa wanandoa hapo ambapo Juma Selemani alikuwa akipinga kitendo cha mke wake(Suzana Elias) kuishi nyumbani kwake na mtoto Justina Laurent (marehemu) na alikuwa akimtaka mkewe ampeleke kwa baba yake mzazi kwani yeye alikuwa akidai hawezi kukaa na kumtunza mtoto ambaye sio wake .

Kaimu Kamanda wa jeshi la polisi wa Mkoa wa Katavi Mohamed Rashid amethibitisha kutokea kwa tukio hilo la kusikitisha.

Alisema wanandoa hao wote wawili wanashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi utakapo kuwa umekamilika.
 
 Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527