Angalia Picha!! HII NDIYO BUNDUKI ILIYOTUMIKA KUTUNGUA HELKOPTA HUKO SIMIYU,WAHUSIKA WAKAMATWA,YUMO MGANGA WA JADI,ALITOA DAWA WASIKAMATWE NA POLISI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu Lazaro Mambosasa akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani) Bunduki aina ya Riffle Na 7209460 CAR Na 63229, iliyotumika kuangusha helkopta na kumuua rubani wake Rodgers Gower (37) raia wa uingereza katika tukio lililotokea ndani ya pori la akiba Maswa wilayani Meatu Mkoani Simiyu.


 
Siku chache baada ya kutokea tukio la majangili katika pori la akiba Maswa wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, kuitungua ndege (Helkopita) iliyokuwa doria na kuawa kwa rubani wake Rodgers Gower (37) watu 9 wamekamatwa kuhusika na tukio hilo.


Katika watuhumiwa hao mmoja alikuwa akifanya kazi katika hifadhi ya Ngororo kitengo cha Interejensia, ambaye alitajwa kuwa mhusika Mkuu wa kufanikisha tukio hilo sambamba na kukamatwa mganga wa jadi.


Akitoa taarifa mbele za waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa polisi Mkoani hapa Lazaro Mambosasa alisema kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi, pamoja na uongozi wa TANAPA.


Kamanda Mambosasa alisema watuhumiwa wote walikamatwa na kukiri kuhusika na tukio hilo, huku akieleza kuwa msako mkubwa uliofanywa na jeshi hilo mara baada ya tukio kutokea chini ya Mkuu wa upelelezi Mkoa Jonathan Shana.


Alisema katika msako huo baadhi ya watuhumiwa walibainika kuwa kiungo kikubwa kufanikisha tukio hilo kwa kutoa mbinu za uharifu, huku wakijihusisha na matukio ya ujangili kwa muda mrefu.


Aliongeza kuwa baadhi yao walibainika kuwa waganga wa jadi, ambapo walikuwa wakitoa dawa kwa majangili za kuosha silaha, ikiwa pamoja kuosha na kusafisha mihili yao ili wasiwe kukamatwa.


Mambosasa aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Shija Mjika (38), Njile Gonga (28) Mhazabe, Masasi Mandago (48) pamoja na Dotto Pangali (41) , ambao ndiyo waliohusika kutungua helkopta hiyo.


Wengine ni Iddi Mashaka (49) ambaye Kamanda Mambosasa alimtaja kuwa aliwahi kufanya kazi katika hifadhi ya Taifa Ngorongoro Kitengo cha Intelijensia na ndiye alikuwa kiungo Mkuu wa tukio hilo.


Aliwataja wengine kuwa ni Mapolu Njige (50) ambaye ni mganga wa jadi aiyekuwa anatumika kutoa dawa za kutokamatwa kwa majangili hao, Mwigulu Kanga (40) , Dotto Huya (45) , Pamoja na Mange Balumu.


Aidha Mambosasa alisema kuwa Mtuhumiwa Dotto Pangali alikamatiwa katika wilaya ya Kishapu Mkoa wa Shinyanga mnamo tarehe 7/02/216 na kufanyiwa upekuzi nyumbani kwake ambapo alikutwa na bunduki aina ya Riffle yenye namba .7209460 CAR Na.63229.


Mkuu huyo wa polisi alisema Mtuhumiwa huyo alikiri bunduki hiyo kutumika katika tukio la kuuawa kwa rubani huyo, ambapo ilibainika kuwa bunduki hiyo inamilikiwa na Mange Magima ambaye pia amekamatwa.


Alisema msako uliendelea nyumbani kwa Pangali na kufanikiwa kukamatwa kwa bunduki nyingine aina ya Riffle Na3478 CAR 458 ikiwa na risasi 6 ambayo ilibainika kumilikiwa na Nghomango Jilala ambaye mpaka sasa hajakamatwa.


Alieleza kuwa jeshi hilo liliendelea kupata taarifa ambapo mnamo tarehe 29/01/2016 walikamatwa Shija Mjika, Njile Gonga, pamoja na Masasi Mandago wakiwa na meno ya tembo 2 yakiwa na uzito wa Kilo 31 yakiwa yamefichwa chini ya daraja katika kijiji cha Itaba.


Aidha Mambosasa alieleza kuwa baada ya kukamatwa kwa wahusika wote ilibainika kuwa bunduki zilizotumika katika tukio hilo zinamilikiwa kihalali na watu ambao waliomba kuzimiliki kwa ajili kujilinda.


“ Mbali na tukio hilo bunduki nyingi wamiliki wake wanawahasimisha majangili kwa ajili ya kutumika kwa uharifu pamoja na kuua wanyama ndani ya hifadhi…lakini na hao wamiliki wanalipwa pesa baada ya uhalifu kufanyika” ,alisema.Alisema baada ya kubaini hilo kulifanyika msako mwingine kwa wanaomiliki silaha, ambapo alisema asilimia kubwa wanaishi karibu na hifadhi, na jumla ya bunduki 27 zimekamatwa na mara baada ya uchunguzi wamiliki watarudishiwa.


“ Tunajiandaa kupeleka zuio la silaha mahakamani ili kubaini kama wana sifa za umiliki…lakini mbali na hilo sasa kutaanzishwa oparesheni kwa watu wote wanaomiliki silaha hasa maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kuwanyanganya”, alisema .


Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa upelelezi juu ya tukio hilo umekamilika na watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kesho  ili kujibu tuhuma zinazowakabili, ambapo alioomba mahakama kuharakisha hukumu kwa vile uchunguzi umekamilika.

Kwa upande wake Mhifadhi mkuu wa Serengeti William Mwakilema amelipongeza jeshi la polisi ambapo amesema tukio hilo lilipotokea liliwasikitisha sana kwani hasara ilipatikana kutokana na kutunguliwa kwa helkopta.
Mnamo tarehe 29/01/2016 saa 11:30 jioni katika eneo la Gululu lililopo ndani ya hifadhi ya Maswa kata ya Mwangudo wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu, watu walidhaniwa kuwa majangili waliipiga risasi ndege (helkopta) 88HFCG iliyokuwa doria na kusababisha kifo cha rubani wake Rodgers Gower (37) raia wa uingereza huku Mwenzake Nicholas Beste (43) raia wa Afrika Kusini akinususrika kifo. 
 Baadhi ya silaha zilizokamatwa wakati wa msako wa kuwatafuta watuhumiwa wa tukio hilo.
 

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527