WAZIRI JAFO AMTUMBUA JIPU MKURUGENZI WA MANISPAA YA ILEMELA BILA GANZI,AMETUMIA VIBAYA MADARAKA


NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, Suleiman Jafo, amemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauli ya Manispaa ya Ilemela, John Wanga kutokana matumizi mabaya ya madaraka.

Waziri Jafo amefikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa ufujaji wa fedha za ujenzi wa uzio wa halmashauli hiyo ulioghalimu Sh. 347 milioni pamoja na kukaidi kuhamia kwenye nyumba ya Serikali ya Sh. 200 milioni.

Naibu huyo wa Tamisemi alitoa agizo hilo wakati akizungumza na watumishi wa manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, ambako amesema mkurugenzi huyo ameshindwa kuhamia katika nyumba hiyo ambayo inakadiliwa kughalimu Sh. 200 milioni na kusababisha Serikali kuendelea kulipia nyumba anayoishi.

Amesema kuwa licha ya Serikali kutoa agizo mkurugenzi huyo kuhamia katika nyumba hiyo lakini yeye aliendelea kupangishia nyumba nzima inayolipiwa Sh. 2 milioni kwa mwezi licha ya kukamilika kwa nyumba iliyojengwa.

Jafo ambaye pia ni Mbunge wa Kisarawe CCM amesema kuwa katika manispaa hiyo kuna matatizo mengi na kwamba itatumwa kikosi cha uchunguzi kutoka Tamisemi ili kufanya uchunguzi namna ambavyo fedha za ujenzi wa uzio zilivyotumika ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa watakaobainika kuhusika na suala hilo.

“Huu ukuta (uzio) hauwezi kughalimu fedha zote hizo, nyie hata kwa madai yenu mnayosema mlifanya haraka kwa sababu ya uchaguzi sio kweli hamtaweza kushawishi kwa hilo.

“Watanzania wana shida, dawa hospitalini hakuna, wakina mama wanajifungulia chini halafu, milioni 200 imekaa tu haina shughuli yeyote ile, mkurugenzi unapaswa kupisha uchunguzi kufanyika kwanza,” amesema Jafo.

Hata hivyo amesema kuwa ujenzi wa nyumba hiyo ulianza tangu mwaka 2013 lakini mpaka sasa mkurugenzi huyo amekataa kwenda kuishi kwa sababu ya kuwa chini ya kiwango na kwamba ipo katika maeneo hatarishi.

Amesema licha ya uongozi wa manispaa hiyo kujipangia kiwango cha Sh. 2 milioni kwa mwezi,kiwango hicho kipo juu ya kiwango cha serikali cha laki nane.

Kwa upande wake mkurugenzi, Wanga katika kujitetea amesema sababu zilizosababisha kushindwa kuhamia katika nyumba hiyo ni kutokana na kuwa katika eneo hatarishi ikilinganishwa na nafasi yake ya ukurugenzi.

“Waziri (Naibu Waziri Tamisemi) tunafanya kazi kubwa za wananchi na kazi zetu mnazifahamu tunafanya watu wengine hawapendi tunachokifanya, sasa nikihamia katika nyumba ile na ukilinganisha na eneo ilipo ni hatari,” amesema Wanga.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527